NA JOHN BUKUKU- TABORA

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni zake mkoani Tabora leo Septemba 12, 2025, ambapo ameahidi ujenzi wa barabara kubwa ya mzunguko (Ring Road) yenye urefu wa kilomita 82 kuzunguka mji wa Tabora.

Amesema ujenzi huo utakwenda sambamba na madaraja 133 ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo.

Aidha, Dkt. Samia amesema serikali imeongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kutoka shilingi bilioni 700 hadi trilioni 1.9 kwa mwaka, ili kuboresha zaidi mtandao wa barabara za vijijini na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.

“Serikali imeona umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye barabara za vijijini kwa sababu ndizo zinazowagusa wananchi moja kwa moja katika shughuli zao za kila siku, hususan wakulima na wafanyabiashara wadogo,” amesema.

Mbali na sekta ya barabara, Dkt. Samia pia ameahidi ujenzi wa kituo cha kudhibiti na kupokea umeme eneo la Ziba, wilayani Igunga, ambacho kitaimarisha upatikanaji wa nishati. Aidha, ameeleza kuwa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Tabora umefikia asilimia 95 na kitakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa zaidi.

Kuhusu sekta ya kilimo, amesema ruzuku za pembejeo na mbolea zitaendelea kutolewa, sambamba na ujenzi wa majosho, minada na chanjo kwa mifugo. Pia amebainisha kuwa serikali itaendelea na ukarabati wa skimu za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji mara mbili kwa mwaka.

Katika sekta ya maji, Dkt. Samia amesema miradi mikubwa ikiwemo ule wa maji kutoka Ziwa Victoria na mingine 28 inaendelea kutekelezwa ili kufanikisha upatikanaji wa maji unaofikia sasa wastani wa asilimia 67.

Vilevile, alibainisha kuwa miradi ya kitaifa kama bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga pamoja na reli ya kisasa ya SGR kipande cha Makutupora–Tabora–Isaka itapita mkoani humo, na kutoa fursa za ajira na biashara kwa wananchi.

Aidha, ameeleza kuwa serikali itafunga taa 2,500 za barabarani katika manispaa na wilaya za Tabora ili kuwezesha wananchi kufanya biashara zao masaa 24.