**************************
NA MWAMVUA MWINYI,RUFIJI
WALIMU wa shule ya Sekondari ya Kata ya Mbwara ,Jimbo la Rufiji Mkoani Pwani, wameweka umeme katika vyumba vya madarasa shuleni hapo pamoja na nyumba wanazoishi kwa gharama ya sh.milioni tatu ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa umeme iliyokuwepo .
Juhudi hiyo ,itasaidia kuinua taaluma kwa wanafunzi wa shule hiyo ,kwani wanaweza kujisomea nyakati za usiku .
Mwalimu Mkuu shuleni ya sekondari Mbwara, Millo Msovela, akieleza juu ya suala hilo wakati mbunge wa viti maalum mkoani Pwani Zainab Vullu alipokwenda kuzungumza na wanafunzi na walimu shuleni hapo,alisema kwasasa changamoto ya ukosefu wa umeme imebakia katika mabweni ya wasichana.
“Hatua hii imetokana na mafundi wa Tanesco kufika kijijini hapa na kuweka miundombinu hiyo, wakati shule ikiwa haina pesa, Mabweni ya wasichana, ilishindikana kutokana na kukosa shilingi laki nne za kuunganishia huduma hiyo,”alieleza Millo.
Aidha alisema, pia shule inadaiwa sh. milioni kumi na Mzabuni aliyetengeneza vitanda 40 kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi 80 wa kike, kati ya 188 waliopo shuleni hapo ukiachilia mbali wavulana 162 wanaosoma kwenye shule hiyo ambapo wanatokea majumbani mwao.
Mbunge wa jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa, alipongeza hatua ya walimu kujichangisha fedha na kuvuta umeme, huku akiahidi kushirikiana na viongozi wenzake ili kurejesha fedha hizo na kuweka umeme katika eneo la mabweni ambalo limesalia.
“Katika taarifa ya mwalimu imegusia changamoto ya deni la vitanda, nitawasiliana na taasisi ya TEA iliyoratibu mradi husika, kuhusu umeme katika mabweni nimewasiliana na meneja wa Tanesco ameniahidi ndani ya wiki mbili umeme utawaka hapa” alisema Mchengerwa.
Nae Zaynab Vullu kabla ya kwenda kukabidhi vifaa tiba kwenye zahanati ya Kijiji cha Mbwara, akiwa shuleni hapo alikabidhi magodoro kumi, huku akiahidi mifuko mitano ya saruji ambapo ameunga mkono mifuko 15 iliyoaihidiwa na Mchengerwa kwa lengo la kukarabati sakafu kwenye majengo shuleni humo.
Vullu hakusita kukemea mimba za shuleni na kuwaasa wanafunzi wa kike kuachana na vishawishi na tamaa za kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi wakiwa shuleni, rift za bodaboda na chips na badala yake wajali masomo kwa manufaa yao ya baadae.