Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tatu kulia) akipiga makofi baada ya kuzindua mnara wa mawasiliano kwenye kijiji cha Mavuji wilayani Kilwa. Wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Dkt. Joseph Kilongola
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tatu kulia) akipata maelezo kuhusu mtambo wa mnara wa mawasiliano kutoka kwa Mhandisi wa TIGO, Willey Kato baada ya kuzindua mnara huo katika kijiji cha Mavuji wilayani Kilwa
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiyagai akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye baada ya kuzinduliwa kwa mnara wa mawasiliano kwenye kijiji cha Mavuji wilayani humo
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedastus Ngombale akiishukuru Serikali kwa kujenga mnara wa mawasiliano kwenye kijiji cha Mavuji kilichopo wilayani Kilwa kabla ya kuzinduliwa kwa mnara huo na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tatu kushoto)
Asha Abdallah Gongo, mkazi wa kijiji cha Mavuji wilayani Kilwa akieleza furaha ya kupata mawasiliano baada ya Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kushoto) kuzindua mnara mpya wa mawasiliano kijijini hapo. Anayesikiliza wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa TIGO wa mikoa ya Pwani, Christopher Mutalemwa
Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungala akiishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Mavuji wilayani Kilwa (hawapo pichani) kabla ya kuzinduliwa kwa mnara wa mawasiliano kwenye kijijini hicho. Katikati ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Christopher Ngubiyagai
……………………………………………………………………………………………………….
- Wananchi wasema hawapandi tena vichuguu kupata mawasiliano
Na Prisca Ulomi, WUUM, Kliwa
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema mawasiliano hayabagui wala hayachagui kwa kuwa Serikali inatoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa ajili ya kujenga minara ya mawasiliano ili wananchi waweze kuwasiliana muda wote
Nditiye ameyasema hayo kwa wananchi wa kijiji cha Mavuji kilichopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi kabla ya kuzindua mnara wa mawasiliano uliojengwa na kampuni ya simu ya TIGO baada ya kupewa ruzuku na UCSAF kujenga mnara huo
Nditiye amesema kuwa mawasiliano hayachagui wala hayabagui, Serikali inahudumia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa walizonazo bali inahakikisha wananchi wanawasiliana na Serikali inataka wananchi watumie simu kuwasiliana
“Wananchi niwatoe hofu na msiogope maneno ya Bungeni ya wabunge wa vyama tofauti kwa kuwa tukitoka nje ya Bunge tunaongea na kunywa chai pamoja,” amesema Nditiye
Pia amezitaka kampuni za simu za mkononi zilizopewa ruzuku na Serikali ya kujenga minara ya mawasiliano kuwa tayari muda wowote anapotaka kwenda kuzindua mnara kwa kuwa Serikali inafanya kazi saa 24 na inatekeleza Ilani ya CCM ambapo hadi sasa asilimia 95.2 ya wananchi wanawasiliana
Naye Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungala ameishukuru Serikali kwa kujenga mnara wa mawasiliano na kusema kuwa sasa kijiji cha Mavuji wananchi wanawasiliana na sasa wanapiga simu wanavyotaka tofauti na zamani ilikuwa mpaka wakajitege ili kupata mawasiliano
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anasema CCM haichagui haibagui, mnara huu wa mawasiliano uliozinduliwa leo unatumiwa na watu wote wawe wanachama wa CCM, CUF, CHADEMA na chama chochote, huu ni utekelazaji wa sera za Serikali na Ilani ya CCM,” amesisitiza Bungala
Pia, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedastus Ngombale ameiomba Serikali kuzindua mnara uliopo jimboni kwake na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lijenge minara kwenye vijiji vilivyopo jimboni kwake kama ilivyoahidi
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiyagai amemshukuru Nditiye kwa kufika kijijini hapo na kuzindua mnara huo bila kujali kuwa ni siku ya jumapili ya mapumziko bali amejali kuwahudumia wananchi
Ngubiyagai ameiomba Serikali kuboresha mawasiliano kwenye Wilaya hiyo kwa kuwa kati ya vijiji 90 zilivyopo wilayani humo, vijiji 20 mawasiliano yake sio mazuri.
Pia, amesema kuwa anaomba Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliopita wilaayani humo uunganishwe kwa kiwango cha kutosha ukilinganisha na hali ilivyo sasa ambapo mtandao uko chini kwenye ofisi za Serikali za Wilaya hiyo ili kuwawezesha watumishi wa umma kutuma taarifa za Serikali kwenye mtandao bila kulazimika kwenda mbali kupata huduma ya mtandao
Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake wa Mavuji baada ya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano, Asia Kijogelo amesema kuwa awali walikuwa wanaenda kupanda kichuguu kupata mawasiliano, ila sasa wanaishukuru Serikali kwa kuwa wamepata mawasiliano ya uhakika
Naye Mkurugenzi wa TIGO wa mikoa ya Pwani, Christopher Mutalemwa amesema kuwa kampuni za simu zimepata fursa ya kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi baada ya Serikali kuunganisha nguvu na kujenga minara kwa kuwa maeneo mengine kampuni za simu haziwezi kupeleka mawasiliano peke yao inabidi washirikiane na Serikali
Akiwasilimu wananchi, Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF, Dkt. Joseph Kilongola amesema kuwa UCSAF kwa kushirikiana na wawekezaji, kampuni za simu za mkononi wanahakikisha kuwa wananchi wanafikiwa na huduma za mawasiliano