Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa Mabwepande waliofika ofisni kwake Dar es Salaam kwa ajili ya kutatua mgogoro wa ardhi kupitia program ya Funguka kwa Waziri jana tarehe 23 Februari 2020.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa Mabwepande waliofika ofisni kwake Dar es Salaam kwa ajili ya kutatua mgogoro wa ardhi kupitia program ya Funguka kwa Waziri jana tarehe 23 Februari 2020.
Sehemu ya wananchi wa jiji la Dar es Salaam waliojitokeza kuonana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa migogoro yao kupitia program ya Funguka kwa Waziri jana tarehe 23 Februari 2020. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
****************************
Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amepongezwa na wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa uamuzi wake wa kukutana nao na kutatua migogoro ya ardhi 628 katika mkoa huo katika kipindi cha siku tano kupitia progaramu ya Funguka kwa Waziri hadi saa nne usiku.
Lukuvi alihitimisha programu ya Funguka kwa Waziri kwa kukutana na wananchi wa Manispaa ya Kinondoni jana tarehe 22 Februari kwa kusikiliza na kutatua kero, malalamiko na migogoro mia tatu (300) iliyomfikisha saa 4:22 usiku.
Awali, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alikutana na wananchi wa Manispaa za Ilala ambapo alishughulikia migogoro 122, Ubungo 75, Kigamboni migogoro 65 na Manispaa ya Temeke migogoro 66 na kufanya jumla ya migogoro aliyoishughulikia kwa siku zote tano kufikia 628.
Kati ya Wananchi aliokutana nao tangu kuanza kwa program hiyo siku ya jumanne tarehe 18 Februari 2020, Manispaa ya Kinondoni ilioonekana kuwa na idadi kubwa ya wananchi wenye malalamiko ya ardhi ukilinganisha na Manispaa nyingine za mkoa wa Dar es Salaam.
Baadhi ya Wananchi waliokutana na Waziri Lukuvi walionesha kufurahishwa na utaratibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kukutana na wananchi kwa nia ya kupata suluhu ya migogoro ya ardhi iliyoelezwa kuwa imekuwa ikiwahangaisha kwa muda mrefu bila mafanikio.
Raphael Ngowi mkazi wa Kinondoni ambaye malalamiko yake ni kuhusiana na kiwanja chake kumilikishwa kwa watu wawili alisema, utaratibu wa Waziri wa Ardhi kukutana moja kwa moja na wananchi unamsaidia kupata mambo mengi kutoka kwa mhusika badala ya kusikia kutoka kwa watendaji.
Alisema, utaratibu huo siyo tu unasaidia wananchi wenye matatizo ama kudhulumiwa haki zao katika sekta ya ardhi bali unatoa pia fursa kwa Waziri mwenye dhamana ya ardhi kubainia uzembe wa baadhi ya watendaji wake katika maeneo yenye migogoro.
Kwa mujibu wa Ngowi, kati ya Mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano, Lukuvi amevunja rekodi kwa kuweza kutatua matatizo ya wananchi kwa kukutana nao ana kwa ana jambo alilolieleza kuwa limeasisiwa na Mwl. Nyerere kwa kuweka uwazi wa kushugulikia kero.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya wenye Mashamba eneo la Mabwepande katika manispaa ya Kinondoni Seif Maungu anayewakilisha wananchi 258 walio katika mgogoro wa kuvamiwa eneo lao alisema, baada ya kuonana na Waziri Lukuvi sasa wamepata faraja kubwa baada ya mateso ya takriban miaka 13.
‘’Kwa muda mrefu tulikuwa hatupati majibu kuhusiana na mgogoro wa maeneo yetu lakini sasa baada ya kukutana na mhe. Lukuvi tumepata faraja na Rais Magufuli amepata jembe’’ alisema Maungu.
Mkazi mwingine wa Magomeni aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Maulid Kinyogoli aliyewasilisha tatizo lake la kutopata Hati ya Ardhi, aliilezea program ya Funguka kwa Waziri kuwa ni mwarobaini wa matatizo ya ardhi yanayosababishwa na watendaji wa sekta ya ardhi wasiokuwa waaminifu.
‘’Utaratibu wa Funguka kwa Waziri uliaonzishwa na Lukuvi kwa kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi ungekuwa ukifanywa na viongozi wengine kupitia sekta zao basi matatizo yangepungua na hivyo kumrahisishia kazi Rais John Pombe Magufuli ya kuleta maendeleo’’ Alisema Kinyogoli.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekuwa na utaratibu wa kukutana na wananchi wenye malalamiko na kero za ardhi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kwa nia ya kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi ambapo tayari program hiyo imeshafanyika mikoa mbalimbali ikiwemo Kilimanjaro, Tanga, Rukwa, Mbeya, Iringa, Tabora, Kigoma, Kagera, Katavi na Lindi na kuleta mafanikio makubwa.