Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
Agosti 26, 2025
Akisukumwa na dhamira ya dhati ya kulitumikia Jimbo la Bagamoyo kwa kutumia taaluma na uzoefu wake serikalini, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, CPA Subira Mgalu, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania Ubunge wa Jimbo hilo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mgalu amesema uamuzi wake wa kugombea unatokana na mwito wa kutumikia wananchi kwa karibu zaidi, akitumia utaalamu wake katika ukaguzi wa fedha kuhakikisha uwazi, usimamizi wa miradi ya maendeleo, na matumizi bora ya rasilimali za umma katika Jimbo hilo muhimu kihistoria na kimaendeleo.
“Nimeguswa na kiu ya maendeleo ya wananchi wa Bagamoyo,Nimetafakari kwa kina, nimeona kuna haja ya kusimama mstari wa mbele katika kusimamia fedha za serikali kuu na mapato ya ndani ya Halmashauri, kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa – ya kuleta huduma bora kwa wananchi,” alisema CPA Mgalu akizungumza baada ya kuchukua fomu katika Ofisi ya Tume Huru ya Uchaguzi Wilaya ya Bagamoyo.
Akiwa katika Viwanja vya CCM Bagamoyo, Mgalu alieleza kuwa pia amesukumwa kugombea kutokana na imani kubwa aliyonayo kwa uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuonyesha njia ya mageuzi katika sekta mbalimbali kupitia serikali ya awamu ya sita.
“Nataka kuwa sehemu ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Bagamoyo kwa kusimamia miradi ya maji, elimu, afya, utalii, barabara, na kuwawezesha wananchi kiuchumi,” aliongeza.
Aidha, aliahidi kuwa kiongozi wa wananchi wote, atakayefungua milango kwa ushauri kutoka kwa wananchi, viongozi wa dini, na hata wabunge waliomtangulia akiwemo Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Shukuru Kawambwa na Muharami Mkenge.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, Abubakary Mlawa, alieleza sasa ni wakati wa mshikamano na si mashindano ya vijembe.
Alitoa wito kwa wanachama wote wa chama hicho kukipigania CCM ishinde kwa kishindo uchaguzi wa mwaka huu.

