Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu (aliyevaa kitenge) akipokelewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mhe. Agnes Mchome wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, baada ya kuwasili leo katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo Kigamboni iliyopo jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu (kushoto) akitembelea Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni iliyopo jijini Dar es Salaam, ambapo alijifunza kuhusu ujenzi wa Mahakama hiyo kwa kutumia gharama nafuu na yenye mazingira rafiki. Katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma na wa kwanza ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mhe. Agnes Mchome wa Mahakama ya Wilaya ya Kigmboni, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Magreth Kinabo- Mahakama)
………………………………………………………………………………………………..
Na Magreth Kinabo na Tawani Salum- Mahakama
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu amesema kwamba amefurahishwa na utendaji kazi wa uwazi wa Mahakama ya Tanzania, ikiwemo huduma ya Mahakama Inayotembea kwa kuwa urahisisha hutoaji haki kwa wakati.
Mhe. Mengistu alitoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea Mahakama Inayotembea iliyokuwa ikitoa huduma kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, eneo Luguruni Mbezi na Mahakama ya Wilaya Kigamboni zilizopo jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Ethiopia alifurahishwa na Mahakama Inayotembea kwa jinsi inavyofanya kazi na kusema kuwa inasaidia kuondoa mlundikano wa mashauri yaliyopo ndani ya Mahakama pia husaidia kutoa huduma za Kimahakama sehemu ambazo hazina Mahakama, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya siku tatu.
‘‘Mahakama ni suluhisho tosha la umalizwaji wa mashauri ndani ya Mahakama’’ pia vifaa vilivyopo ndani kwa mfano kuwepo kifaa maalum cha kuwapandishia walemavu hii Mahakama imezingatia wenzetu walemavu na kuwa hii ni ishara tosha kuwa sasa Mahakama imedhamiria kuwa karibu na wananchi,” alisema Jaji Mkuu huyo.
Aliongeza kuwa kufanya ziara hapa nchini Tanzania ni baada ya kuona kuwa Mahakama ya Tanzania ina maboresho makubwa hivyo basi hakuweza kujiuliza mara mbili kuja kutembelea Mahakama ya Tanzania hasa kutokana na kasi ya umalizwaji wa mashauri, ujengwaji wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) husaidia kumalizwaji wa mashauri kwa wakati.
“Nimefurahishwa na maboresho makubwa, ukiwemo utendaji kazi wa uwazi’’ alisisitiza.
Naye Mhe. Moses Ndelwa ambaye ni Mratibu wa Mahakama Inayotembea, alisema Mahakama hiyo, imeendelea kusikiliza mashauri kwa ngazi ya Mahakama ya Mwanzo. Hivyo kwa upande wa jiji la Mwanza mashauri 57 yalifunguliwa na kutolewa uamuzi.
Aliongeza kwamba katika jiji la Dar es Salaam mashauri 92 yalifunguliwa na kusikilizwa. Pia mashauri yote yamesikilizwa na kutolewa uamuzi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
“Kwa mwananchi anayehitaji kufungua shauri la madai, anaweza kufungua katika Mahakama Inayotembea kama madai yake yanathamani isiyozidi shilingi milioni hamsini (Tzs. 50,000,000/=). Mashauri yanaweza kufunguliwa mojamoja katika gari la Mahakama Inayotembea au katika Mahakama ya Mwanzo inayopatikana karibu na kituo ambacho Mahakama Inayotembea inatoa huduma.
Ndelwa alifafanua kuwa imekuwa ikisikiliza mashauri ya jinai yanayotokana na operesheni maalumu, ambapo jumla ya watuhumiwa 184 walifikishwa katika Mahakama inayotembea, mashauri yalisikilizwa ndani ya siku moja na kutolewa uamuazi.
Alisema mbali na usikilizaji wa mashauri, inatoa huduma nyingine kama vile kutoa fomu za kiapo, kuthibitisha nyaraka mbalimbali, kutoa fomu za kufungulia mashauri, kutoa nakala za hukumu, kupokea malalamiko na kutoa vipeperushi pamoja na taarifa mbalimbali zinazohusu Mahakama.
Mpaka sasa takribani wananchi 97 wamepata huduma mbalimbali za kimahakama kupitia Mahakama Inayotembea.
Kwa upande wa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Agnes Mchome alisema Mahakama hiyo katika kipindi cha mwaka 2019 mashauri yaliyofunguliwa ni 318, yaliyotolewa uamuzi 250 na yaliyobakia ni 186.
Wakati huohuo, Jaji Mkuu huyo alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) ambacho pia kinachohusisha Mahakimu na kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi wao.