Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo Pichani) jijini Dar es Salaam leo tarehe 18 Februari 2020 kutoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya Kjamii kuhusiana na kuporwa kwa ardhi ya wananchi na viongozi wa umma katika eneo la Ununio Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam. Kulia ni Kamishna wa Ardhi nchini Methew Nhonge na kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kaskazini Leo Komba.
*********************************
Na Munir Shemweta, WANMM DAR ES SALAAM
Serikali imekanusha taarifa ya kuporwa ardhi ya wananchi na viongozi wa umma kilichokuwa kiwanja NA 11 Eneo la Ununio katika Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam kama ilivyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Akikanusha kuporwa kwa eneo hilo leo jijini Dar es Salaam mbele wa waandishi wa Habari, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kuporwa kwa eneo hilo siyo za kweli kwa kuwa eneo hilo lilishabatilishwa kwa mujibu wa fungu la 48 (3) la sheria ya ardhi Na 4 (1999).
Makondo aliwaasa wananchi kuipuuza taarifa hiyo kwa kuwa ina lengo la kuwachafua viongozi na kubainisha kuwa, kwa mujibu wa sheria ya ardhi namba 4 (1999) Kamishna wa Ardhi anayo mamlaka kisheria kumilikisha ardhi kwa Mtanzania yoyote aliyetimiza masharti kisheria.
Akifafanua kuhusiana na suala hilo Kamishna wa Ardhi Nchini Mathew Nhonge alisema eneo linalodaiwa kuporwa lilipimwa kwa mara ya kwanza mwaka 1988 na kuitwa kiwanja namba 11 eneo la Ununio.
Nhonge alisema, mwaka 1988 Manispaa ya Kinondoni ilimilikisha kiwanja hicho kwa Ndg Goodfreid Kajana Makaya na kupewa Hati NA 43711 ambapo baadaye kulijitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wakidai kuwa ni wenyeji wa eneo hilo akiwemo Ramadhani Mwinyihamisi, Waziri Kibosha na Bi Kijakazi Maulid.
Kamishana huyo wa Ardhi nchini alibainisha kuwa, malalmiko hayo yalisababisha mgogoro uliofikishwa Makahakama kuu Kitengo cha Ardhi kupitia Shauri la Ardhi NA 93/2004 baina ya Bi Kijakazi Maulid dhidi ya mmiliki halali Ndg Goodfreid Kajana Makaya ambapo hata hivyo shauri hilo lilitupiliwa mbali na Mahakama hiyo baada ya Bi. Kijakazi kushindwa kuthibitisha madai yake.
Nhonge aliongeza kwa kusema, mwaka 2007 Ndg Goodfreid Kajana Makaya alihamisha umiliki wake kisheria kwa kuiuzia Kampuni ya Shamiana Builders Limited aliyoieleza kuwa nayo ilishindwa kutekeleza masharti ya uendelezaji kama ilivyoelelekezwa kwenye hati miliki na hivyo kusababisha haki ya umiliki kufutwa mwaka 2017 na serikali kwa mujibu wa fungu la 48 (3) la sheria ya ardhi Na 4 (1999).
Kufuatia hali hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ililipanga na hatimaye kulipima upya eneo hilo na takribana viwanja 22 vilipatikana na kumilikishwa kwa wananchi mbalimbali wakiwemo wakazi wa Uninio ambao maombi yao ya kumilikishwa yaliwasilishwa serikalini.