Na Hellen Mtereko,
Mwanza
Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza wakikabiliwa na jumla ya mashtaka matano yanayohusiana na uhalifu wa kiuchumi, likiwemo kosa la kuongoza genge la uhalifu na kukutwa na noti bandia.
Washitakiwa hao ni Richard Jackson Sinkala (38) mkazi wa Buhongwa, Hassan Ibrahim (47) mkazi wa Igoma, Emmanuel Simon Ngama (32) mkazi wa Nyahong’homango, na Gerald Melijory Majaliwa (30) mkazi wa Buhongwa, Jijini Mwanza. Walifikishwa mahakamani leo Julia 30,2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Erick Malrley, ambapo mashtaka yao yalisomwa na Wakili wa Serikali Sileo Mazullah.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kosa la kwanza linawahusisha wote wanne kwa kuongoza genge la uhalifu, kinyume na Kifungu cha 4(1), 57(1), na 61(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (Marejeo ya 2023). Kosa la pili ni kukutwa na noti zilizoghushiwa, kinyume na Kifungu cha 348 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya 2023).
Kosa la tatu linamhusu mshtakiwa wa kwanza peke yake, ambaye anadaiwa kufoji noti, kinyume na Kifungu cha 338 cha Kanuni hiyo hiyo. Kosa la nne ni utakatishaji wa fedha dhidi ya mshtakiwa wa kwanza, kinyume na Kifungu cha 12(c) na 13(1)(a) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 423 (Marejeo ya 2023), vikisomwa pamoja na Kifungu cha 57(1) na 61(2) vya Sura ya 200.
Kosa la tano linawahusu washtakiwa wote wanne kwa tuhuma za utakatishaji wa fedha, wakidaiwa kukiuka masharti ya kifungu hicho hicho cha sheria pamoja na Aya ya 22 ya Jedwali la Kwanza.
Makosa hayo yanadaiwa kutendeka kati ya Januari 2023 hadi Julai 17, 2025, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Erick Malrley aliwaeleza washtakiwa kutojibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo mpaka kibali kitakapowasilishwa. Hivyo, aliagiza warejeshwe Gereza la Butimba hadi Agosti 13, 2025, kesi itakapotajwa tena.