Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Simiyu Mhandisi Albert Kent, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara ya Maswa – Bariadi (km 49.7), kwa kiwango cha lami, mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Simiyu Mhandisi Albert
Kent, kuhusu umuhimu wa kuzingatia ubora unaoendana na thamani ya fedha zinazotolewa katika ujenzi wa barabara ya Maswa – Bariadi (km 49.7), kwa kiwango cha lami, mkoani Simiyu.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Maswa – Bariadi (km 49.7),
inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Simiyu. Barabara hii
inagharamiwa na fedha za ndani kwa gharama ya shilingi bilioni 86.99.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akimkaribisha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya kukagua athari za mvua katika miundombinu ya barabara na
madaraja, mkoani Simiyu.
***********************
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ametoa wito kwa watanzania wote kutoa taarifa katika Mamlaka za Serikali zinazohusika kuhusu maeneo yote yenye changamoto iwe ni kwenye madaraja au barabara ambazo
zimeharibika kutokana na mvua nyingi za mwaka huu.
Naibu Waziri Kwandikwa ametoa wito huo mara baada ya kuwasili mkoani Simiyu katika ziara yake ya kikazi ya kukagua athari zilizotokana na mvua kubwa zilizonyesha katika kipindi cha mwisho wa mwaka na zile za mwanzo mwa mwaka huu katika miundombinu ya barabara ambayo
imekamilika na ile inayoendelea kutekelezwa.
“Niwaombe watanzania wenzangu mjue kuwa Serikali yenu haipendi mpate shida mahali kwahiyo mkiona sehemu barabara au madaraja yana changamoto toeni taarifa hizo katika Mamlaka husika na vitashughulikiwa
haraka zaidi iwezekanavyo”. Amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua mradi wa ujenzi unaoendelea wa barabara ya Maswa – Bariadi (km 49.7) kwa kiwango cha lami na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo mpaka sasa umefikia asilimia 78.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa hatua hizi za maendeleo za mradi huu unatokana na kodi za wananchi na kuwapongeza watanzania kwa kuendelea kuunga mkono Serikali yao kwa kulipa kodi na hivyo kurahisisha
maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Hii barabara inagharamiwa na fedha za ndani hivyo niwahakikishie kuwa kodi zenu ndio matunda ya miundombinu bora na imara, uboreshaji wa
afya, Elimu na mambo mengine mengi ya kimaendeleo”. Amefafanua Naibu Waziri Kwandikwa.
Mapema akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Simiyu Mhandisi Albert Kent, ameeleza kuwa mradi huo mpaka sasa jumla ya kilometa 17.3 zimekamilika kujengwa
kwa kiwango cha lami na magari yameruhusiwa kupita ili kuepusha usumbufu hasa vipindi hivi vya mvua.
Mhandisi Kent amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kuusimamia mradi huo ambao unatakiwa ukamilike mwezi Septemba mwaka huu kwa kuzingatia ubora unaoendana na thamani ya fedha zilizotolewa.
“Mkandarasi anaendelea vizuri na kazi ya ujenzi yakiwemo madaraja makubwa mawili (Daraja la Simiyu na Banhya) na mengine madogo madogo pamoja na ujenzi wa tuta la barabara katika maeneo mbalimbali”. Amesema Mhandisi Kent.
Naibu Waziri Kwandikwa yupo katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Simiyu unaohudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 923.65 ambapo kilometa 334.33 ni barabara kuu, kilometa 521.62 barabarab za mkoa na kilometa 67.7 ni za barabara ya Wilaya ya Nkoma – Makao iliyokasimiwa.