Dkt. Leonard Subi akijibu maswali kutoka kwa wajumbe walioshiriki kikao jijini dodoma na wale walioshiriki kikao hicho kwa njia ya mtandao jijini Dar es salaam
Baadhi ya washiriki wa kikao cha tathimini ya mpango wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma wakifuatilia mada zilizowasilishwa kwenye kikao cha tathimini
Mkurugenzi wa idara ya kinga Dkt. Leonard Subi akifungua kikao cha mapitio na tathimini ya mpango wa taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma kwenye ukumbi wa takwimu jijini dodoma.
***************************
Na. Catherine Sungura-Dodoma
Serikali kupitia wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto imeweza kupiga hatua kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kugundua wenye kifua kikuu(TB) nchini kwa ongezeko la asilimia 18.
Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Dkt. Leonard Subi wakati akifungua kikao cha mapitio na tathimini wa mpango wa taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma(NTLP) ambao unajumuisha wadau mbalimbali wa kifua kikuu nchini.
“Kikao hiki ni cha mapitio na tathimini wa mpango mkakati wa miaka mitano ambao unatimilika mwaka huu,tumekuwa tukifanya mapitio haya kila baada ya miaka mitano hadi sita ambapo mwaka 2014 tuliweza kujitathimini tuna uwezo gani wa kupambana dhidi ya kifua kikuu na ukoma”.
Dkt. Subi amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kwani uwezo wa kugundua TB umeongezeka kutoka asilimia 37 mwaka 2015 hadi asilimia 53 ya wagonjwa wanaokadiriwa kuwa na kifua kikuumwaka 2018.
“Lakini vifo vitokanavyo na kifua kikuu vimepungua kwa zaidi ya asilimia 27,haya ni mafanikio makubwa sana ya mpango huu”.alisema
Aidha, Dkt. Subi amesema licha ya mafanikio hayo hivi sasa wameongeza uwezo wa kuchungua TB kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa kutumia kipimo cha kielectroniki (Gene-Expert Mashine) ambapo wizara imeweza kununua mashine zipatazo 239 na kuzisambaza kwenye vituo vya afya vya msingi nchi nzima ambavyo vipimo hivyo vinatoa majibu ya mgonjwa ndani ya masaa wawali tofauti na zamani walipokuwa wakitumia harubini na kutoa majibu kwa zaidi ya masaa arobaini na nane.
Hata hivyo alisema kupitia elimu ya afya kwa umma ambayo hutolewa na wizara kupitia NTLP hivyo wananchi wanaelewa na imesaidia kupungua kwa magonjwa haya na watu kwenda vituo vya kutolea huduma kwa uchunguzi na matibabu.
“Tanzania ni nchi mojawapo imefanikiwa kulingana na malengo ya kimataifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwani tunaonesha muelekeo mzuri kwa kasi ambayo tumeionyesha kwenye kifua kikuu”.
Kwa upande wa ugonjwa wa ukoma Mkurugenzi huyo amesema kuwa nchi imefikia kiwango cha kuondosha ukoma kabisa na kubakiza halmashauri kumi na sita,takribani wagonjwa 2000 (elfu mbili) wanakadiriwa kuwa na ugonjwa huo nchi nzima hivyo wanaendelea na mkakati wa kuhakikisha kuwafikia wagonjwa wote na kuwatibu ili kupunguza madhara ambayo wamekuwa wakiyapata ikiwemo ulemavu.
Tathimini hiyo itafanyika kwenye baadhi ya mikoa ambayo italeta matokeo na changamoto ili kutengeneza mpango mkakati mwingine wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 ili kuweza kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya kifua kikuu.