Mratibu wa kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole kulia,akiongea na mmoja wa mzazi Hawa Hemed mwenye mtoto aliyebainika kupata maradhi ya kifua kikuu wakati wa kampeni ya uchunguzi na upimaji wa TB iliyofanyika katika Hospitali ya Misheni Mbesa wilayani humo,
Muhudumu wa Afya ngazi ya jamii Salum anajihusisha na uelimishaji kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu wilayani Tunduru Salum Kalembo akiongea jana na baadhi ya akina mama wa kijiji cha Mbesa waliofika kwenye kampeni ya uchunguzi na upimaji wa ugonjwa wa kifua kikuu wilayani Tunduru katika Hospitali ya Misheni Mbesa.
Mratibu wa kifau kikuu na ukoma kutoka Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akitoa elimu ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa baadhi ya akina mama wa kijiji cha Mbesa walifika katika zoezi la uchunguzi na upimaji wa ugonjwa huo iliyofanyika katika Hospitali ya Misheni Mbesa katika kampeni maalum ya kutokomeza ugonjwa huo ambayo wilaya ya Tunduru imezindua kampeni kabambe inayojulikana kama Nyumba kwa nyumba,shule kwa shule na Kilinge kwa Kilinge ambayo inalenga kumaliza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2035.
Picha na Mpia Picha Wetu
*****************************
Na Mwandishi Wetu,
Tunduru
TATIZO la utapia mlo linalotokana na ukosefu wa lishe bora kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano linatajwa kuchangia kuongezeka kwa ugonjwa wa kifua kikuu ambao unapoteza maisha ya watoto wengi hapa nchini.
Hivyo,wazazi na walezi wameaswa kuhakikisha wanawapatia watoto wao mlo kamili,mlo bora na kuzingatia kanuni bora za Afya kama njia mojawapo ya kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Mratibu wa kitengo cha kifua kikuu na Ukoma katika Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole amesema hayo jana,wakati kampeni ya uelimishaji,uchunguzi na upimaji wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa watoto iliyofanyika katika Hospitali ya Misheni Mbesa.
Kampeni inayojulikana kwa jina la nyumba kwa nyumba,shule kwa shule na kilinge kwa kilinge ni mkakati wa wilaya kwa kushirikiana na Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kumaliza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Alisema, mtoto mwenye Utapia mlo yuko katika hatari kubwa ya kupata maradhi ya kifua kikuu,kwa hiyo njia pekee ya kuwakinga wasipate maradhi ni wazazi na jamii kuwapatia lishe bora mara kwa mara na kuwafikisha katika maeneo ya kutolea huduma kwa ajili ya uchunguzi pindi wanapoona mabadiliko ya afya za watoto hao.
Alisema, kifua kikuu na ugonjwa hatari ambao unashambulia sehemu zote za mwili wa binadamu na mgonjwa mmoja wa kifua kikuu awe mtoto mdogo au mtu mzima anaweza kuambukiza watu kati ya kumi hadi kumi na tano kwa mwaka,hivyo ni hatari sana kwa maisha ya watu wengine katika jamii.
Dkt Kihongole alisema,njia pekee itakayosaidia kukomesha maradhi hayo ni jamii yote kuhakikisha wanashiriki na kujitokeza kwa wingi katika kampeni ya upimaji iliyozinduliwa tangu Mwezi Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dkt Kihongole,ugonjwa wa kifua kikuu ni chanzo kikubwa cha umaskini katika familia hasa ikizingatia kuwa mgonjwa wa kifua kikuu ambaye hajaanza tiba kimsingi hawezi kushiriki vema katika shughuli za uzalishaji mali kwani atakuwa anasumbuliwa na homa mara kwa mara.
Katika hatua nyingine, Kihongole ameitaka jamii kuacha kuwatenga wagonjwa wa kifua kikuu kwani mgonjwa aliyeanza matibabu hawezi tena kuambukiza watu wengine na kusisitiza kuwapa ushirikiano wagonjwa wa kifua kikuu na kuhakikisha wale ambao hawajaanza matibabu kuwapeleka katika maeneo ya kutolea huduma kupata matibabu.
Alisema, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani WHO iko katika mpango kabambe ya kuhakikisha inatokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Alisema, katika kuunga mkono juhudi hizo za Serikali na shirika la Afya Duniani WHO, Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu imejipanga kuendelea na kampeni ya uelimishaji,upimaji wa nyumba kwa nyumba,shule kwa shule na kilinge kwa kilinge na hakuna mwananchi hatakayeachwa bila kupimwa.
Alisema katika kampeni hiyo, Hospitali ya wilaya kupitia kitengo chake cha kifua kikuu na Ukoma imeanza kuwatumia waganga wa tiba asili na tiba mabadala kuibua watu wanaofika kwenye vilinge kupata tiba kwa wale wanaoonekana kuwa na viashiria vya kifua kikuu kuwahimiza kwenda Hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa Afya zao.
Kwa hiyo,ameitaka jamii kuwapa ushirikiano mkubwa waganga wa Tiba asili pindi wanapokwenda katika vilinge kwani tangu walipoanza kushirikishwa katika kampeni hiyo mwaka jana kumekuwa na mafanikio makubwa ya kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu na kuwaonya wazazi kuacha kuwakatisha dawa watoto walioanza matibabu ya kifua kikuu na kusisitiza kuwa mzazi atakaye bainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
“wazazi lazima mkumbuke kuwa hawa watoto sio wenu ni wa Serikali,ndiyo maana wanapatiwa huduma zote za matibabu bure hadi wanapokuwa wazima,kwa hiyo msijaribu kwa namna yoyote kuwakatisha dawa kwani athari yake ni kubwa sana”alisema Kihongole.
Mmoja wa wazazi Ali Taliko alisema, elimu aliyoipata kuhusiana na kifua kikuu itasaidia kuokoa maisha ya mtoto wake na watoto wengine katika jamii ambao wanasumbuliwa na maradhi hayo kwa muda mrefu hata hivyo wameshindwa kupata majawabu kutokana na kukosa uelewa.
Alisema, baada ya kufikiwa na huduma na kubaini tatizo la mtoto wake,atahakikisha anasimamia vizuri matibabu ya mtoto wake na kuwa Balozi mzuri kwa wazazi wengine na kuishukuru Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kufanya kampeni hiyo ambayo itakwenda kusaidia na kuokoa maisha ya watoto wengi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni Mbesa Dkt Masaga Mzelifa ameipongeza Serikali kwa kuendesha kampeni hiyo ambayo kimsingi itasaidia sana kupunguza tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi wa kata ya Mbesa na wilaya ya Tunduru.
Alisema, wao kama sehemu ya wadau muhimu wa masuala ya Afya wanapokea na kutoa matibabu kwa watu wanaobainika kuwa na ugonjwa huo,hata hivyo changamoto kubwa ni upungufu wa baadhi ya vifaa hasa vile vinavyotumika kuchunguza vimelea vya vya ugonjwa huo.
Aidha alitaja changamoto nyingine ni ukosefu wa wodi maalum ya kulaza wagonjwa wa kifua kikuu ambapo alieleza kuwa, kama kungepatikana wodi hiyo ingekuwa rahisi kuwaweka pamoja wagonjwa hao na kuwapatia matibabu.