Ruvuma.
Ugin Mkinga ni jina jipya lenye mvuto mkubwa katika anga ya siasa ya Tanzania, hasa kwa wale wanaofuatilia mustakabali wa maendeleo ya Jimbo la Madaba, Huyu ni kijana mzalendo mwenye ari, maarifa ya kimataifa na moyo wa kujitolea, ambaye sasa amejitosa rasmi katika kuwania Ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), akilenga kulihudumia jimbo alilotokea kwa moyo mmoja.
Safari yake ya kisiasa si ya bahati nasibu bali ya asili, kwani Ugin alizaliwa kwenye familia ya kisiasa. Mama yake alikuwa mwanzilishi wa kata maarufu ya Temeke na alihudumu kama Diwani wa Kurasini, jambo lililomlea Ugin katika mazingira ya uongozi, uwajibikaji na siasa ya ukweli tangu akiwa mdogo.
Kwa zaidi ya miaka 18 Ugin ameishi nchini Australia, ambako alipata maarifa ya hali ya juu, uzoefu mpana na mtazamo wa kimataifa kuhusu maendeleo ya jamii. Akiwa huko, aliendelea kubeba uzalendo wake kwa moyo wote na ndoto yake ilikuwa ni kurudi nyumbani kuwatumikia watu wa Madaba.
Jina la Ugin Mkinga limeanza kuwa gumzo ndani ya Jimbo la Madaba, hasa baada ya kuanzisha taasisi ya Mkinga Foundation, ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi, hasa wale wa kipato cha chini, Kupitia taasisi hii, amewagusa wengi kwa huduma za kijamii zisizo na masharti.
Ni mzaliwa halisi wa Madaba Kijiji cha Mahanje, na amekulia Mabanda Kata ya Lilondo, na ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Msingi Lilondo. Ukaribu wake na jamii unadhihirisha kuwa anafahamu matatizo yao, changamoto zao, na ndoto zao na yuko tayari kuwa sehemu ya suluhisho.
Ugin si tu mwanasiasa, bali ni kiongozi mwenye uwezo wa kiutendaji, akiwa na sifa ya kuwa Facilitator anayejua kusimamia, kuratibu, na kufanikisha miradi ya maendeleo. Anaamini kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji uongozi wenye dira, uwazi na ushirikishwaji wa wananchi.
Anatambua kuwa “charity begins at home”, kauli inayomuongoza kuwekeza muda na rasilimali zake kwenye jamii aliyozaliwa. Hili linaonyesha kwamba nia yake si ya kisiasa tu bali ni wito wa dhati wa kulitumikia eneo lake la asili.
Mkinga anakuja na maono makubwa ya kuibadilisha Madaba, kuwa jimbo linalojitegemea kwa kutumia rasilimali zake, anaamini kuwa kwa kushirikiana na serikali, chama na wananchi, Madaba inaweza kuwa kitovu cha maendeleo kusini mwa Tanzania.
Uwezo wake wa kuwasiliana na watu wa rika zote unamtofautisha na wengi. Anaelewa lugha ya vijana, wazee, wanawake na makundi maalum, na anawapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jimbo.
Anapigania maendeleo jumuishi yanayogusa kila mwananchi. Ajenda yake haijajikita kwenye miundombinu pekee, bali pia kwenye elimu bora, afya, ajira kwa vijana na uwezeshaji wa wanawake sekta ambazo kwa muda mrefu zimehitaji msukumo mpya katika jimbo hilo.
Uaminifu wake katika chama chake cha CCM hauna mashaka, Ni mwana CCM wa kweli ambaye anaelewa misingi ya chama na falsafa ya viongozi waliotangulia kama Mwalimu Julius Nyerere na hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye alimuinua kifikra kuhusu dhana ya utumishi uliotukuka.
Ugin Mkinga anajua kuwa maendeleo si ya mtu mmoja, bali ni matokeo ya mshikamano. Kwa mantiki hiyo, amejipanga kushirikiana na viongozi wa serikali na chama ili kuhakikisha kuwa kila mtu anakuwa sehemu ya mafanikio ya Madaba.
Moja ya malengo yake makubwa ni kuunganisha jimbo lote kisiasa, kijamii na kiuchumi. Analenga kuondoa migawanyiko isiyo ya lazima na kuhamasisha mshikamano wa kudumu kati ya vijiji na kata zote za Madaba.
Ni kiongozi anayesikiliza, anayejifunza na anayetekeleza. Kauli zake zimejaa unyenyekevu lakini pia zimebeba matumaini mapya kwa watu wa Madaba ana matumaini ya maendeleo yasiyokuwa na ubaguzi wa aina yoyote.
Ni mgombea anayekuja na mipango kabambe ya kuinua kilimo cha kisasa, kufungua masoko ya mazao ya wakulima na kuongeza thamani ya bidhaa zao. Anaelewa kuwa uchumi wa Madaba unategemea kilimo, hivyo atahakikisha sekta hiyo inapata msukumo mkubwa.
Katika sekta ya elimu, ameahidi kuwekeza kwa nguvu, kujenga madarasa bora, kusaidia vifaa vya kujifunzia na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wa Madaba wanapata elimu bora kama watoto wa mijini.
Uaminifu wake, uadilifu na moyo wa kujitolea vimewavutia wananchi wengi wa Madaba. Wengi wanasema, “Huyu si mwanasiasa wa maneno, bali wa vitendo,” kwani matendo yake tayari yameonekana kabla hata ya kupewa nafasi ya uongozi rasmi.
Ugin Mkinga anaelewa fika kuwa uongozi ni dhamana. Ameahidi kutanguliza maslahi ya wananchi mbele ya maslahi binafsi, na kuhakikisha kuwa kila senti ya rasilimali ya umma inatumika kwa ufanisi na kwa uwazi.
Mwalimu Jailos Wilson Ndali: Ushuhuda wa Malezi na Uongozi wa Ugin Mkinga
Mwalimu Jailos Wilson Ndali, aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Lilondo katika Halmashauri ya Madaba tangu mwaka 1978, anakumbuka kwa hisia kubwa namna alivyomkaribisha Ugin Mkinga kujiunga na darasa la kwanza mwaka 1980.
Wakati huo, Ugin alikuwa akiishi na babu yake, huku wazazi wake wakiishi jijini Dar es Salaam,
Kwa kuzingatia mazingira hayo wazazi wa Ugin walimkabidhi rasmi mwalimu Ndali jukumu la kumsimamia kijana wao katika masomo na malezi shuleni hapo.
Baada ya muda, Mwalimu Ndali alihamia kufundisha katika Shule ya Msingi Tuliani, lakini kumbukumbu ya Ugin haikumtoka. Anaeleza kuwa Ugin alikuwa mwanafunzi hodari, mwenye bidii na aliyeshiriki kikamilifu katika shughuli zote za shule. Alijitokeza kuwa kiongozi kijana tangu akiwa mdogo, jambo ambalo lilimtofautisha na wenzake.
Mwalimu Ndali anasema kuwa uongozi wa Ugin ni wa kuzaliwa, jambo linalodhihirishwa na maadili mema na malezi bora aliyoyapata kutoka kwa wazazi wake. Mama yake alikuwa mtendaji wa serikali, huku baba yake akiwa mwanajeshi na hali iliyomjengea msingi wa uwajibikaji, nidhamu na kujituma.
Mwalimu Ndali anasema anamtakia Ugin Mkinga kila la heri katika safari yake mpya ya kisiasa, na ana imani kuwa kutokana na bidii yake na moyo wa kujitolea, ataweza kuwatumikia wana Madaba kwa ufanisi na kuwaletea maendeleo endelevu.
Kwa ujumla, Ugin Mkinga ni kiongozi wa kizazi kipya mwenye mchanganyiko wa ujuzi wa kimataifa, uzalendo wa kweli na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Madaba. Kama chama kitampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM, ni dhahiri kuwa Jimbo la Madaba litakuwa na mwakilishi wa watu, sio tu kwa jina, bali kwa vitendo.