NA DENIS MLOWE IRINGA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassimu Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za msimu wa nne wa Great Ruaha Marathon itakayofanyika katika Mbuga za Ruaha Julai 5 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari na kamati ya maandalizi ya mbio hizo, Mkuu wa mkoa wa Iringa, Kheri James alisema kuwa mbio hizi hazilengi tu ushindani wa riadha bali pia zinachochea juhudi za kukuza utalii wa Kusini.
Alisema kuwa mbio za Great Ruaha Marathon ni zaidi ya Mbio kwani ina nafasi kubwa ya kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, hususan katika maeneo ya vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkubwa.
Kheri James, amesema serikali ipo tayari kuhakikisha mbio hizo zinafanyika kwa usalama, amani na mafanikio makubwa huku akiwaomba wakazi wa Iringa na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo za kipekee ambazo zinatangaza utalii wa Nyanda za Juu Kusini.
“Aliongeza kuwa Mbio za Great Ruaha Marathon ni za aina yake kwa sababu binadamu na wanyama wanapishana katika mazingira moja kwa amani ni tukio la kipekee linalopaswa kutangazwa na hii ya kwanza nchini.
Kwa upande wake Mratibu wa Great Marathon, Hamim Kilahama, amesema maandalizi yanaendelea vizuri huku usajili ukiwa na mwitikio mkubwa ambapo zaidi ya watu 350 wamekwishajisajiri.
Ameongeza kuwa mbali na mbio hizo kutakuwa pia na utalii wa kipekee kama vile sport fishing, utalii wa kutembea, na hivyo kuwakaribisha Watanzania na wageni kutoka nje kujitokeza kwa wingi.
“Ruaha Great Marathon si tukio la kawaida ni sherehe ya utalii, mazingira na afya inayowakutanisha wanariadha na wapenda mazingira ndani ya moja ya hifadhi kubwa na nzuri zaidi barani Afrika” alisema
Katika mbio hizo licha ya uwepo wa waziri mkuu wengine wanaotarajiwa kuwepo ni mawaziri mbalimbali,wakuu wa mikoa Wakurugenzi na klabu mbalimbali za wakimbiaji nchini.



