Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.

Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, akimkaribisha Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, ili aweze kufungua mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.

Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Janeth Hiza, akizungumza wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, wakifuatilia mawasilisho mbalimbali wakati wa mafunzo kwa Waratibu hao yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, yaliyofanyika jijini Dodoma.

Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja (katikati) akisikiliza baadhi ya michango iliyokua inatolewa na washiriki wa mafunzo yaliyohusisha Wizara ya Fedha na Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri Bi. Evelyine Mangweha, akiuliza swali wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Dionisia Mjema na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.

Mchumi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Felista Malibate, akitoa mada kuhusu Kanuni za Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mwaka 2019 wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.

Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha wa Manispaa ya Ubungo, Bi.Evelyine Mangweha, akichangia mada wakati wa mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha yaliyofanyika jijini Dodoma.

Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, baada ya kumalizika kwa halfa ya ufunguzi, iliyofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dodoma)
Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma
Serikali imewataka Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha nchini kuongeza kasi, ubunifu na weledi katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mifumo rasmi ya kifedha inayotambulika na kusimamiwa na Serikali ili kuhakikisha wanapata maarifa yatakayowawezesha kujikwamua kiuchumi kwa njia salama na endelevu.
Agizo hilo limetolewa na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, wakati akufungua mafunzo maalum kwa Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyolenga kuwawezesha waratibu hao kutoa elimu sahihi kwa jamii wanazozihudumia.
Dkt. Mwamwaja alisisitiza umuhimu wa kutumia mafunzo hayo kama jukwaa la kubadilishana mawazo, uzoefu na mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazowakabili waratibu hao katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Maarifa haya msiyabakize kwenye makabrasha, pelekeni kwa wananchi waelimisheni waelewe faida ya kutumia mifumo rasmi ya kifedha kama benki, SACCOS, VICOBA vilivyosajiliwa na taasisi zingine zilizo chini ya uangalizi wa Serikali kwa kuwa ndiyo njia salama ya kuwasaidia kuinuka kiuchumi,” alisema Dkt. Mwamwaja.
Aliongeza kuwa mafanikio ya sekta hiyo hayatategemea tu uwepo wa Sera, Sheria na Kanuni nzuri, bali yanategemea zaidi utekelezaji wenye tija, weledi, uwajibikaji na ufuatiliaji makini unaoanzia kwa Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha ambao ndio kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kufikisha elimu na huduma bora za kifedha.
Aidha, aliwapongeza Waratibu wote kwa kujitokeza kwa wingi na kwa wakati katika mafunzo hayo, na kuwataka kuyachukulia kama fursa ya kuimarisha uwezo wao wa kuwaelimisha wananchi kwa njia shirikishi, rafiki na yenye matokeo chanya.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Mohamed Nyange, alisema kuwa mafunzo hayo yamewapa maarifa ya kina na mbinu sahihi zitakazowawezesha kuwafikia wananchi kwa ufanisi, kutoa elimu inayoeleweka, na kusaidia jamii kuelewa umuhimu wa kutumia huduma rasmi za kifedha kwa maendeleo yao ya kiuchumi.
“Ili tuweze kutoa elimu sahihi kwa wananchi tunaowahudumia lazima nasi tuwe na uelewa wa kutosha kwanza, niwapongeze Wizara ya Fedha kwa kutujengea uwezo huu, tutaenda kutumia maarifa haya kwa kuhakikisha wananchi wetu wanajua, wanaelewa na wanatumia huduma za kifedha rasmi kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi,” alisema Bw. Nyange.
Mafunzo haya yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), lengo ni kuhakikisha nchi inakuwa na mtandao mpana wa waratibu waliobobea katika kutoa elimu ya kifedha kwa jamii.
Serikali imeendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo watendaji wake ili kuhakikisha elimu ya fedha inamfikia kila Mtanzania, kupitia elimu hiyo, wananchi wataweza kufanya maamuzi sahihi ya kifedha ikiwemo kutumia mifumo rasmi inayotambuliwa na Serikali kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Jumla ya mikoa 13 imeshiriki katika mafunzo hayo, ambayo ni: Mbeya, Pwani, Njombe, Shinyanga, Dar es Salaam, Tanga, Singida, Morogoro, Dodoma, Simiyu, Iringa, Arusha na Kilimanjaro.