NA DENIS MLOWE IRINGA
Mkuu wa wilaya ya Kilolo Rebecca Msemwa ambaye alimwakilisha mkuu wa wilaya ya Iringa Kheri James ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Iringa amewataka vijana kuchangamkia mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri zao na kuacha kulalamika hawana mitaji.
Msemwa alisema hayo wakati alipokuwa mgeni Rasmi katika kongamano la wamiliki wa Saloon na wafanyakazi mkoani hapa kuwa serikali kupitia halmashauri wanatoa mikopo ambayo haina riba hivyo ni wakati wao kujiunga katika vikundi mbalimbali na kufikisha maombi yao kwa afisa maendeleo wa jamii
Alisema kuwa katika hili atawasimamia vyema kuweza kupata mikopo hiyo na atasikitika sana kuona vijana wanaendelea kulalamika hawana mikopo wakati serikali inatoa bila riba.
Alisema kuwa awali mikopo ilikuwa ikitolewa kwa vijana chini ya miaka 34 lakini alipoingia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan aliongeza umri hadi kufikia miaka 45 wanaruhusiwa kupata mikopo hivyo muhimu wananchi kujitokeza kuomba mikopo hiyo.
Aliwapongeza wamiliki wa Saloon na wafanyakazi na kuwataka kuthamini ajira hiyo kwani imekuwa mkombozi kwa watu wengi katika suala la usafi.
Aliwataka kuthamini ajira hiyo kwani kwa sasa ni tegemeo kwa kila mtu hata viongozi lazima watumie Saloon kujipendezesha wanachotakiwa kuzingatia ubora wa mazingira yao wanayofanyia usafi ili kuongeza thamani yao.
Kwa upande wake Wakili Moses Ambindwile alitoa wito kwa taasisi binafsi na taasisi za umma kuangalia namna ya kusaidia tasnia ya usukaji na unyoaji (saloon) kama chanzo kikubwa cha mapato kwa nchi.
Alisema kuwa endapo fani hiyo itarasimishwa rasmi utakuwa moja ya vyanzo vikuu vya mapato na kuifanya kuwa bora zaidi kuliko ilivyo sasa.
Alisema kuwa taasisi binafsi na za umma zikiwekeza katika kuwasaidia wafanyakazi wa Saloon zitabadilisha kwa kiasi kikubwa mwenekano wa Saloon na kutolea mfano taasisi za kibenki zikitoa mikopo ya kuwawezesha Saloon kuwa kubwa na ubora chanzo cha mapato kitakuwa na kuongeza ajira kwa vijana.
Wakili Ambindwile alisema kuwa ili kutimiza vigezo kuwe chama ambacho kitaendelee kusimamia misingi na mikataba ya wafanyakazi wa Saloon ili kuwe na usimamizi madhubuti ambao utasimamia ubora wa Saloon.
Alisema kuwa endapo litafanyika hilo kutasababisha viwango vya bei ambavyo havipishani na kuongeza kuwa saloon ziwekewe hadi ngazi za Saloon kinyota kwani ni rahisi kuweka bei kutokana na ubora wake.
Aliongeza kila kuwa katika katiba ya nchi ya mwaka ya 1977 ibara ya 22 inaweka haki ya kufanya kazi kwa kila mwananchi hivyo watu wa Saloon Wengi mnaendesha pasipo kuwa na mikataba Sheria za nchi zinakwenda mbali zaidi na kuna Sheria zinazoonyesha mahusiano ya ajira hivyo kuna umuhimu wa kurasimisha Saloon na kupata heshima wekeni mikataba kwa wafanyakazi .
Alitoa rai pia kwa wamiliki na waajiri kupitia umoja na mikutano muhimu kujua haki zenu kwa njia ya mikataba ambayo itatawala mahusiano na kufanya sekta ambayo itaheshimika kwa kiasi kikubwa nchini kwani kila mtu anategemea kuwa msafi kupitia Saloon.
Wakili Ambindwile alitoa wito pia kwa vijana hao katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kwani vijana wana haki haki ya kushiriki uchaguzi mkuu katika kupiga kura na gombea nafasi mbalimbali.
Hivyo kwa kuuonyesha uimara wenu kwa kuzingatia nini katiba inataka katika uchaguzi mkuu nendeni mkachague viongozi ambao watawatoa mahali mliopo katika kuelekea maendeleo mnayotaka.