Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Kisare Makori katikati akikata utepe kabla ya kukabidhi malori mawili(Tiprer)yaliyonunuliwa na Halmashauri ya Wilaya Mbinga ili kurahisisha utekelezaji wa miradi na kuboresha huduma za kijamii katika Halmashauri hiyo,kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Joseph Kashushura.
Na Mwandishi Maalum,Mbinga
HALMASHAURI ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,imenunua magari mawili ya mizigo(Tipper) yatakayosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri,kutoa ajira kwa vijana,kurahisisha utekelezaji na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Malori hayo yenye usajili SM 43931 na SM 43932, yana ukubwa wa mita za ujazo 19 yamenunuliwa kwa Sh.milioni 380 fedha kutoka mapato ya ndani na fedha nyingine Sh.milioni 15 zimetumika kulipia Bima.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Joseph Kashushura amesema,ununuzi wa magari hayo ni mkakati wa Halmashauri wa kuongeza mapato kwa kutumia rasilimali zake badala ya kutegemea vyanzo vya nje.
Aidha alisema,magari hayo yatasaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi kwa kusogeza vifaa kwa wakati na kupunguza gharama kubwa za ujenzi wa miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga.
“malori haya mawili yatatumika katika shughuli kama usafirishaji wa vifaa vya ujenzi na huduma mbalimbali hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi”alisema Kashushura.
Kwa mujibu wa Kashushura,Serikali imekuwa inaleta fedha nyingi katika Halmashauri na mifumo ya utekelezaji ni wake ni kuwatumia mafundi wadogo na wakandarasi, lakini ili kuepuka gharama kubwa menejimenti ya Halmashauri ikaona ni vizuri kuwa na vitendea kazi vyake.
Alisema,kupitia magari hayo wana uhakika watapunguza gharama za ujenzi na hata miradi husika itatekelezwa na kukamilika kwa wakati na kuhudumia wananchi waliopo katika Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Makori Kisare,ameipongeza Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa kununua magri hayo ambayo yanakwenda kuongeza mapato ya Halmashauri kuchochea uchumi na maendeleo ya wananchi na Wilaya ya Mbinga kwa ujumla.
Makori alisema,magari hayo yatasaidia kwenye kutekeleza miradi kwa ufanisi na tija na Serikali ya Wilaya inafarijika kuona namna Halmashauri hiyo inavyoendelea kupiga hatua kubwa.
Amewataka, kutunza magari hayo na kuhakikisha yanafanya kazi iliyokusudiwa hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu badala ya kutumia kinyume na malengo.
Prisca Haule mkazi wa Litumbandyosi ,ameipongeza Halmashauri kwa hatua hiyo akisema,itaongeza ajira na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii.
Aliongeza kuwa,magari hayo ni sehemu ya mipango ya Halmashauri kuongeza mapato na kurahisisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi kwa kuwa yatatumika kubeba vifaa vya ujenzi kupeleka kwenye miradi inayotekelezwa mbali na maeneo ya mjini.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Kisare Makori,akimkabidhi funguo ya magari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Josepg Kashushuru yaliyonunuliwa kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo,kushoto aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Desdelius Haule.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Kisare Makori katikati akikata utepe kabla ya kukabidhi malori mawili(Tiprer)yaliyonunuliwa na Halmashauri ya Wilaya Mbinga ili kurahisisha utekelezaji wa miradi na kuboresha huduma za kijamii katika Halmashauri hiyo,kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Joseph Kashushura.