Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba,akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR),Sarah Masasi,wakionesha Mkataba ,wakati wa hafla hiyo, iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma. Halfa ya utiaji saini mikataba hiyo imeshuhudiwa na Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde.
Na Alex Sonna, DODOMA
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesaini mikataba minne ya kihistoria na kampuni za uchimbaji madini pamoja na viwanda vya kusafisha dhahabu, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha akiba ya fedha za kigeni na usimamizi wa rasilimali za taifa.
Akizungumza leo Juni 16, 2025, jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema tangu kuanza kwa Mpango wa Ununuzi wa Dhahabu mwaka 2022/23, Benki hiyo imefanikiwa kununua kilo 5,022.85 za dhahabu safi zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 554.28. Kiasi hicho kimevuka lengo la mwaka la Dola milioni 350 na kusaidia kuimarisha hifadhi ya fedha za kigeni, sambamba na kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje.
“Dhahabu hii imenunuliwa kupitia viwanda vya usafishaji vilivyopo hapa nchini kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na kwa bei ya ushindani,” alisema Bw. Tutuba na kutaja viwanda hivyo kuwa ni Mwanza Precious Metals Refinery (kilo 3,181.3), Eyes of Africa (kilo 979.5), na Geita Gold Refinery (kilo 385.6).
Aidha, amebainisha kuwa sehemu ya dhahabu hiyo tayari imehifadhiwa katika Benki Kuu ya Uingereza kama sehemu ya akiba ya kimataifa ya taifa.
Hata hivyo, Gavana Tutuba ametaja baadhi ya changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa mpango huo, ikiwemo kutotambuliwa kwa BoT kama mnunuzi wa madini mengine kama fedha (silver) katika sheria ya madini, pamoja na viwanda vya ndani kutopata ithibati ya kimataifa ya LBMA. Alitoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kurekebisha sheria hizo na kuondoa vikwazo vya kodi vinavyoathiri usafirishaji na uhifadhi wa dhahabu.
Amesisitiza kuwa BoT itaendelea kuwa mshirika wa kudumu na wa kuaminika katika sekta ya madini, huku akihimiza ushirikiano baina ya sekta za madini, fedha na sheria kwa ustawi wa taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye alishuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo, amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kuwawezesha wachimbaji wakubwa na wadogo, na kuongeza fedha za kigeni nchini.
“Natoa wito kwa viwanda vya kusafisha dhahabu hapa nchini kuhakikisha vinaongeza uwezo wao wa usafishaji ili kufikia viwango vya kupata ithibati ya kimataifa,” amesema Dkt. Nchemba.
Ameongeza kuwa BoT inapaswa kuendeleza jitihada zake kuhakikisha kufikia lengo la kununua tani sita za dhahabu kutoka kwa wachimbaji nchini ifikapo mwaka 2026.
Kwa upande wake Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa sekta hiyo imeongeza mchango wake kwa pato la Taifa kutoka asilimia 9.0 mwaka 2015 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024/25.
Amefafanua kuwa sekta ya madini ilikuwa inachangia kiasi cha Sh. bilioni 162 mwaka mzima katika Mfuko Mkuu wa Serikali lakini baada ya marekebisho ya Sheria kwa sasa inachangia kiasi cha Sh. bilioni 753 wakati lengo ni kufikia sh. trilioni moja, lengo ambalo alisema litafikiwa.
“Hiki ni kiasi kikubwa kuwahi kutokea na hii inatokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambaye anatuongoza vema katika nchi yetu, kuhakikisha madini yanaongezwa thamani na kuchangia katika Uchumi wa nchi yetu,’’amesema Mhe. Mavunde.
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza wakati wa halfa ya utiaji saini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu kati ya Benki Kuu ya Tanzania na kampuni za Uchimbaji Madini, Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR),iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma.
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza wakati wa halfa ya utiaji saini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu kati ya Benki Kuu ya Tanzania na kampuni za Uchimbaji Madini, Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR),iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Fedha, Mhe.Dkt. Mwigulu Nchemba,akizungumza wakati wa halfa ya utiaji saini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu kati ya Benki Kuu ya Tanzania na kampuni za Uchimbaji Madini, Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR), iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Fedha, Mhe.Dkt. Mwigulu Nchemba,akisisitiza jambo wakati wa halfa ya utiaji saini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu kati ya Benki Kuu ya Tanzania na kampuni za Uchimbaji Madini, Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR), iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde,akizungumza wakati wa halfa ya utiaji saini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu kati ya Benki Kuu ya Tanzania na kampuni za Uchimbaji Madini, Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR), iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki kutoka kampuni za Uchimbaji Madini, Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR),wakifatilia hafla hiyo iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, akitia saini Mikataba ya Ununuzi na usafishaji madini kutoka kampuni za Uchimbaji Madini, Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR), hafla hiyo iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma. Halfa ya utiaji saini mikataba hiyo imeshuhudiwa na Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde.
Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (katikati), Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde (kulia) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Kampuni za Madini na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu baada ya kumaliza kusaini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu, hafl iliyofanyika leo Juni 16,2025 jijini Dodoma.