Washiriki wa mafunzo ya maadili kwa kamati ya Uongozi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst.), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akifungua mafunzo ya maadili kwa kamati ya Uongozi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo. Kushoto ni Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Dkt. Mussa Juma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst.), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya maadili kwa kamati ya Uongozi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo. Kulia kwake ni Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Dkt. Mussa Juma na Naibu Kamishna wa Bima, Bi. Khadija Issa Said (kushoto kwake).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst.), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akiagana na Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Dkt. Mussa Juma baada ya kufungua mafunzo ya maadili kwa kamati ya Uongozi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo.
******************************
Na Happiness Shayo -Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst.) George H. Mkuchika ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuhakikisha kampuni binafsi za bima
nchini zinajiendesha kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu ili kutoa huduma zenye ufanisi na ubora kwa wananchi.
Rai hiyo ameitoa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa Kamati ya Uongozi ya Mamlaka hiyo yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo.
“Kazi yenu ni kuhakikisha kampuni binafsi za bima zinalipa kodi na zinawalipa kwa wakati wananchi wanaopata ajali za moto, ajali ya gari na majanga mengineyo” Mhe. Mkuchika amesema.
Ameielekeza mamlaka hiyo kufanya ufuatiliaji katika baadhi ya kampuni binafsi zinazotumia muda mrefu kuwalipa wateja wanapopatwa na majanga.
“Serikali iliona umuhimu wa kuwa na chombo kinachodhibiti shughuli za bima nchini ili kuwasaidia wananchi wasiotendewa haki wanapofuatilia
stahiki zao baada ya kukumbwa na majanga mbalimbali kwa hiyo nawaomba muwe wakali kuhakikisha wateja wa kampuni hizi wanapata haki zao kwa sababu ninyi ndio kimbilio lao wanapokuwa hawatendewi haki” Mhe. Mkuchika amesema.
Pia, Mhe. Mkuchika ameitaka mamlaka hiyo kusimamia vyema kampuni binafsi ambazo zina matatizo ya mtaji zijiondoe zenyewe ili kupunguza malalamiko ya wananchi wanaodhulumiwa haki zao wakati wa majanga.
Aidha, Mhe. Mkuchika amezikumbusha taasisi na mashirika ya umma nchini kuhakikisha yanatoa gawio kwa Serikali bila kusukumwa kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kutekeleza Utawala Bora.
Naye, Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Dkt. Mussa Juma amesema kuwa mamlaka hiyo itaendelea
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwezesha mchango wa sekta ya bima nchini ili kuongeza pato la taifa ikiwa ni sehemu ya kufuata misingi ya Utawala Bora.
“Mamlaka itatoa kinga ya bima kwa sekta zote za uchumi na wananchi dhidi ya majanga mbalimbali ya kiuchumi na kijamii” Dkt.Juma ameongeza.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania imeandaa mafunzo ya maadili lengo ikiwa ni kuboresha utendaji kazi kwa watumishi wa Mamlaka hiyo, kuongeza ufanisi na tija kwa taasisi hiyo katika kutekeleza sera ya Utawala
Bora. Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wajumbe wa kamati ya uongozi na kamati ya uadilifu kutoka katika Mamlaka hiyo na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.