Naibu Katibu Mkuu(Elimu) OR- TAMISEMI Gerald G. Mweli
*******************************
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
SERIKALI inajenga shule 1,000 mpya za Sekondari ikiwa ni kukabiliana na ongezeko la wanafunzi lililotokana na kuanza kutolewa kwa elimu bila malipo.
Hayo aliyabainisha jijini hapa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (anayeshughulikia elimu), Gerald Mweli alipokuwa akizungumzia mafanikio ya utekelezaji wa elimu bila malipo kwa elimumsingi ulioanzishwa na Rais John Magufuli.
Alisema kupitia programu ya kuboresha elimu ya sekondari, serikali inajenga shule 1,000 mpya ambazo zitasaidia uchukuaji wa wanafunzi wote waliofaulu.
“ Hili suala la kufanya machaguo ya pili kwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari linafika mwisho kwasababu serikali inajenga shule mpya 1,000 za sekondari, achilia mbali zile zinazoboreshwa na kukarabatiwa.”
“ Ikumbukwe pia serikali iliamua kutoa elimu bila malipo kuanzia mwaka 2016 na kulikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliandikishwa elimu ya msingi ambao kwa sasa wako darasa la tano, hivyo ujenzi wa shule mpya pia ni maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hawa.”
Mweli alisema shule hizo zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 kwa kila shule kwa wakati mmoja.
“ Hivyo kwa kujenga shule hizi mpya, ni kuhakikisha kuwa hakuna mtoto ambaye atafaulu atakosa nafasi ya kuendelea na masomo kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa au kukosa shule.”
Alisema Serikali kuanza kutoa elimu bila malipo hakukuanza kwa bahati mbaya, kuna tafiti zilifanyika mwaka 2014/2015 ambazo zilionesha takribani watoto milioni 3.5 walio na umri wa kwenda shule hawako shuleni na moja ya sababu ilikuwa ni wazazi kukosa fedha lakini pia ni katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu.
Aidha, Mweli alisema kwa mwaka huu, mikoa na maeneo ambayo wanafunzi waliofaulu hawakupata nafasi katika chaguo la awali wameamua maeneo hayo wanafunzi wasome kwa zamu katika kipindi cha miezi miwili.
” Sio kweli kuwa wanafunzi watalundikana, kuna maeneo wanafunzi wameongeza wawili watatu, lakini kuna maeneo wataingia kwa zamu na utaratibu kama huu sio mpya hata huko nyuma kulikuwa na wanafunzi wanasoma kwa zamu.”
Alisema hadi kufikia Februari 29 mwaka huu, madarasa yanayojengwa yatakuwa yamekamilika na wanafunzi kuingia kwenye utaratibu wa sasa.
Kwa upande wa shule za msingi, Mweli alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016 mpaka sasa shule mpya za msingi 295 zimejengwa na madarasa 2000 yamejenga.
” Shule ya Msingi ya Majimatitu ya Jijini Dar es Salaam ambayo ilikuwa na idadi kuwa ya wanafunzi walioandikishwa mwaka 2016 ni moja ya shule ambazo zimenufaika na ujenzi wa shule mpya, kuna moja tumejenga eneo hilo lakini shule ya pili tumeijenga aneo ambalo serikal imepewa ekari tatu bure.”
Mweli alisema kabla ya kuanza kutolewa elimu bila malipo uandikishaji wa wanafunziwa elimu ya awali walikuwa ni milioni moja nchi nzima na asilimia 55 ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza walikuwa wakipitia kwenye elimu ya awali.
“ Tangu tuanze kutoa elimu bila malipo wanafunzi wanaoandikishwa elimu ya awali wamefikia wanafunzi 1,295,000 kwa mwaka na asilimia 82 ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza wanakuwa wamepitia kwenye elimu hiyo ambayo inawasaidia katika stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.”