Umeme kutoka TANESCO, Mhandisi John Skauki akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la bwawa la Mtera leo Februari 7, 2020
Umeme kutoka TANESCO, Mhandisi John Skauki akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la bwawa la Mtera leo Februari 7, 2020
……………………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Mtera
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa tahadhari kwa Wananchi wa Vijiji jirani na vyanzo vya kufua umeme kwa maji vya Mtera na Kidatu kufuatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini(TMA) kuwa mvua bado zinaendelea kunyesha na zipo juu ya wastani.
Kufuatia taarifa hiyo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini, Meneja Mwandamizi Uzalishaji Umeme Mhandisi John Skauki amesema wataalamu wa TANESCO wanafanya tathmini iwapo siku za usoni maji yahamie upande wa pili kwa ajili ya usalama wa Bwawa na mitambo.
Alisema Wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari na kuongeza maji hayatakuwa yanasambaa bali yatapita kwenye mkondo wake wa asili ambako wananchi wanafanya shughuli zao za kijamii.
“TANESCO tumeona ni muhimu leo kutoa tahadhari kwa Wananchi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, kwa kawaida Bwawa la Mtera kulijaza huchukua miezi 3 hadi 4 kwa mvua za masika, lakini kwa kipindi hiki mvua za vuli zimekuwa nyingi ndani ya mwezi mmoja kina kimeongezeka”, alisema Mhandisi Skauki.
Alisema tahadhari inatolewa kwa Wananchi kusitisha shughuli zao za kijamii kama uvuvi, kulisha mifugo, kilimo na nyingine kwenye mkondo wa maji au sehemu zenye vidimbwi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Aliongeza kuwa, kawaida kina cha maji kujaa ni mita 698.50 juu ya usawa bahari na kuongeza hivi sasa kina cha maji kimefikia 698.03 juu ya usawa wa bahari.
“Ikitulazimu tutaruhusu maji kwenda upande wa pili, hili ni zoezi la kawaida na halina madhara yoyote kwa jamii, mara ya mwisho maji kuzidi kiwango ilikuwa mwaka 2008 zoezi lilifanyika na hakukuwa na madhara yoyote kwani maji hupita kwenye mkondo wake wa asili”, alisisitiza Mhandisi Skauki.
Aidha, maji yatakapofika kina cha mwisho TANESCO itatolea taarifa aliongeza.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Uhusiano Bi. Leila Muhaji akizungumzia jinsi ambavyo jamii inayoishi kandokando na vyanzo vya maji inahusishwa alisema, TANESCO imekuwa ikitoa elimu kwa Wananchi hao, lakini pia kushirikiana na viongozi wa Vijiji, Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji, Maafisa wa Uvuvi.
“Tumefika hapa kuwatoa hofu Wananchi na hii tunayotoa ni tahadhari tuu kwa Wananchi”, alisema Bi. Muhaji.
Afisa Mtendaji Kata ya Mtera Bi. Naomi Fungulia alisema siku zote wamekuwa wakishirikiana na TANESCO na wamekuwa wakitoa tahadhari kwa wananchi kupitia vikao mbalimbali wanavyovifanya.
Bwawa la Mtera lilijengwa mwaka 1988 na limekuwa likitumika kwenye uzalishaji wa umeme kwa vituo viwili vya Mtera megawati 80 na Kidatu megawati 201.
Vyanzo vya maji vya bwawa la Mtera ni vitatu ambavyo ni Mto wa Ruaha Mkuu, Ruaha Mdogo ambvyo vipo Mkoani Iringa na Mto Kisigo unaopata maji kutokea Mikoa ya Singida na Dodoma.
Kwa hivi sasa bwawa la Mtera ndio bwawa kubwa na linachangia takribani asilimia 30 ya umeme kwenye gridi ya Taifa.
Aidha, inatarajiwa maji ya Mtera pia yatachangia kwenye ufuaji wa umeme bwawa la Nyerere kupitia mto Kilombero, bwawa la Julius Nyerere litakuwa na uwezo wa kufua megawati 2115 za umeme.