Papa Leo XIV alipokuwa Mkuu wa Shirika la watawa wa Agustino Duniani alipotembelea Parokia ya Mahanje na Wino Agosti 2003.
Na Albano Midelo
Katika kijiji kidogo chenye utulivu wa kimungu kilichopo Mahanje,Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kuna chumba cha kawaida – lakini historia yake si ya kawaida hata kidogo.
Ndani ya chumba hiki, miaka 22 iliyopita, alilala mtu ambaye hivi sasa ni Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani – Papa Leo XIV.
Wakati huo hakuwa Papa. Alikuwa Mtawa na Mkuu wa Shirika la Watawa wa Agustino Duniani, akizuru Tanzania katika ziara ya kichungaji. Ilikuwa mwezi Agosti 2003 alipofika Parokia ya Mahanje, ambako alikaa kwa siku nne, na kulala katika chumba hicho kwa siku tatu mfululizo – akiwa pamoja na watawa wenzake wa Shirika hilo.
Kwa macho ya kawaida, ni kitanda cha kawaida, chumba chenye samani zisizong’ara – lakini kwa walio waamini, kwa walio na jicho la imani, hiyo ni alama ya baraka, historia na heshima kubwa kwa Parokia ya Mahanje na Tanzania kwa ujumla.
Papa Leo XIV alikuwepo hapa – kwa miguu yake mwenyewe
“Alipofika hapa, alikaa nasi kama mtawa mnyenyekevu, hakujionesha mtu mkubwa, lakini alikuwa na utulivu wa ajabu na busara ya kiroho iliyovutia wengi,” anasimulia Padre Titus Raphael Kuyela wa Shirika la Mtakatifu Agustino Tanzania, ambaye ni Paroko wa Parokia ya Mahanje.
“Baada ya kuwasili Mahanje, alikaa nasi, akala nasi, akaomba nasi. Siku iliyofuata alikwenda Jimboni kumtembelea Askofu Mtega – aliyekuwa Baba Askofu wa Jimbo la Songea wakati huo. Lakini akarudi tena hapa, na kulala siku tatu katika chumba hiki. Sasa hiki tunakiita chumba cha Papa.”
Kutoka Mahanje hadi Vatican: Safari ya Imani
Hakuna aliyedhani, wala kutarajia, kuwa Mtawa huyo kutoka Marekani angewahi kuwa Baba Mtakatifu wa Kanisa la Kiroma. Lakini historia ikaandika jina lake – na Parokia ya Mahanje ikapata nafasi ya kipekee katika ramani ya historia ya kanisa duniani.
“Tuliposikia ametangazwa kuwa Papa nilishindwa kujizuia. Niliruka kwa furaha, nikamwamsha mwenzangu usiku nikamwambia, ‘Njoo uone, mkuu wetu wa zamani wa shirika amechaguliwa kuwa Papa!’” anasema Padre Kuyela kwa bashasha.
Baada ya kuchaguliwa kuwa Papa, picha zake zilianza kusambaa, baadhi zikiwa ni zile alizopiga akiwa hapa Tanzania – ikiwemo Parokia ya Mahanje na kituo cha Wino Madaba, ambako pia aliwatembelea watawa wa Shirika lake.
Mahanje: Parokia yenye historia ya miaka 100
Parokia ya Mahanje iliyoanzishwa mwaka 1926, mwaka huu wa 2025 inatimiza karne moja ya uwepo wa Ukristo katika eneo hilo. Na sasa, historia yake inajipambanua kwa uzito zaidi – kuwa sehemu ya maisha ya Papa aliye hai.
Hili ni tukio la kiimani, kihistoria, na la kipekee ambalo linapaswa kuwekwa katika kumbukumbu za Kanisa na Taifa. Wengi sasa watafanya hija kwenda kuona kitanda cha Papa – wakiamini kuwa ni eneo la baraka na sala.
Baraka kwa Ruvuma, Baraka kwa Tanzania
Ujio wa Papa Leo XIV kabla ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa juu wa kanisa ni ishara ya heshima ya kiroho kwa nchi yetu. Na kwa watu wa Mahanje, ni tukio linalofungua ukurasa mpya wa imani, historia na utalii wa kidini.
“Ni fahari yetu. Hatukutarajia. Lakini Mungu aliamua kuweka alama yake hapa. Tuko tayari kulinda kumbukumbu hii kwa vizazi vijavyo,” anasema Padre Kuyela.
Katika wakati ambapo dunia inatafuta alama za tumaini, chumba hiki – na hadithi hii – vinaendelea kuwatia moyo wengi. Kwa wakazi wa Mahanje, na kwa Wakatoliki kote duniani, kitanda hiki sasa si cha kawaida tena – ni sehemu ya historia ya Kanisa Katoliki duniani.
Padre Titusi Kuyela wa Shirika la Agustino Tanzania Parokia ya Mahanje Jimbo Kuu la Songea.
Papa Leo XIV alipokuwa Mkuu wa Shirika la watawa wa Agustino Duniani alipotembelea Parokia ya Mahanje na Wino Agosti 2003.
Chumba ambacho alilala Papa Leo XIV akiwa kiongozi wa Shirika la watawa wa Agustino Duniani alilala kwa siku tatu katika Parokia ya Mahanje.
Muonekano wa kanisa la Parokia ya Mahanje Madaba wilayani Songea