Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Stela Tulo akimfafanulia jambo Naibu Msajili Mahakama Kuu Charles Magesa alipotembelea Banda la Msajili wa Mabaraza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square Dodoma leo 04 Feb 2020.
Msajili Msaidizi wa Baraza la Ardhi na Nyumba Kanda ya Kati Shilly Repenti (Kulia) na Afisa Ardhi Anord Mkude wakitoa elimu kwa wateja waliotembelea Banda la Ofisi ya Msajili wa Mabaraza Winfrida Mtengule (Kushoto) na Asha Komba wakati wa Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square Dodoma leo 04 Feb 20202.
Afisa Ardhi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Anold Mkude akimsikiliza kwa makini Wakili Upendo Mwakatika wakati wa Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma leo tarehe 4 Feb 20202 (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).
********************************
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tulo amewataka wananchi kutumia vyombo vilivyo wekwa kwa mujibu wa sheria katika kutafuta haki kwenye migogoro ya ardhi.
Tulo alisema hayo leo tarehe 4 Februari 2020 katika maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Alisema, kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi walio kwenye migogoro ya ardhi kwenda kwa viongozi kama vile Wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wengine kutafuta haki kwenye migogoro ya ardhi na kuacha vyombo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria jambo alilolieleza linachangia migogoro ya ardhi kutapata suluhu kwa wakati.
Kwa mujibu wa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini, vyombo vinavyohusika kisheria kutoa haki katika migogoro ya ardhi ni kuanzia ngazi ya Baraza la Ardhi la Kijiji, Kata, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi na Mahakama ya Rufaa.
Alisema, iwapo wananchi walio kwenye migogoro ya ardhi watafuata utaratibu wa kutumia vyombo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria wataweza kupata haki zao na wakati huo na kuepuka kupoteza muda mwingi wa kukata rufani kuhusiana na migogoro ya ardhi.
Aidha, Tulo alitumia fursa ya Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kuwataka wananchi wa jiji la Dodoma na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho hayo ili kupata elimu kuhusiana na Mabaraza ya Ardhi na hivyo kujua taratibu za kutafuta wakati wa migogoro ya ardhi.
Naye Afisa Ardhi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Arnold Mkude alisema Ofisi ya Msajili wa Mabaraza ya Ardhi nchini inayatumia maonesho ya Wiki ya Sheria kama njia ya kutoa elimu kwa wananchi wote wanaotembelea Banda la ofisi hiyo ili kufahamu kazi na namna Mabaraza ya Ardhi yanavyofanya kazi.
Hata hivyo, alisema tangu kuanza Maonesho hayo wananchi wengi wa,mekuwa wakijitokeza kwenye banda hilo kwa nia ya kutaka kupata ufahamu kuhusiana na Mabaraza ya Ardhi na kubainisha kuwa wengi wao wameonesha kutokuwa na uelewa wa Mabaraza ya Ardhi au taratibu za kufuata wakati wa kushuhulika na migogoro ya ardhi.