Katibu wa UVCCM Singida DC, Zainabu Abdallah akizungumza na baadhi ya watoto waishio kwenye mazingira magumu, kwenye eneo la Shule ya Msingi Ilongelo, Singida DC.
Katibu wa UVCCM Singida DC, Zainabu Abdallah akiwa na baadhi ya watoto waishio kwenye mazingira magumu, kwenye eneo la shule ya Msingi Ilongelo, Singida DC.
Kiongozi huyu wa Umoja wa Vijana akiendelea kukagua kazi mbalimbali za watoto hao yeye na wenzake walipowatembelea shuleni hapo.
Picha ya pamoja baina ya viongozi wa UVCCM wilaya ya singida Vijijini Zainabu Abdallah, Happynes Ahmed, Athumani Musa na walimu wa shule ya msingi Ilongelo na wanafunzi wa makundi yenye mahitaji maalumu baada ya kuwakabidhi zawadi na vifaa mbalimbali jana.
Na Mwandishi Wetu, Singida
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa kimesema kimejipanga vema kuendelea kushika Dola, huku kikiwasihi watanzania kuzidi kukiamini na kukiunga mkono ili kukamilisha azma yake chanya ya kuleta ustawi wa kiuchumi kwa maendeleo endelevu chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM wilayani humo, Zainabu Abdallah aliyasema hayo mara baada ya kuwatembelea watoto wa makundi yenye mahitaji maalumu kwenye baadhi ya shule zilizopo ndani ya halmashauri ya Wilaya ya Singida DC, zoezi lililokwenda sambamba na kuwapatia msaada wa vifaa mbalimbali kwa mahitaji yao-kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 43 tangu kuzaliwa kwa chama hicho.
“Watanzania wote ni mashahidi, chama hiki chini ya Mwenyekiti wetu John Magufuli siku hadi siku kimeendelea kutekeleza ilani yake kwa vitendo…ukizitazama huduma za afya, elimu, miundombinu, sekta ya nishati na nyinginezo nyingi ni dhahiri utabaini nia njema iliyopo ya kufikisha maendeleo ya kweli kwa ustawi wa watu wake wote bila kubagua,” alisema Abdallah.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kukiamini na kukiunga mkono chama hicho ambacho mbali ya kufanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi, lakini pia kipo mbioni kushughulikia baadhi ya kero chache zilizosalia, ikiwemo eneo la miundombinu kwa baadhi ya maeneo, na upatikanaji wa mikopo ya pembejeo ili kuwawezesha wakulima kulima kilimo chenye tija.
“Nyote mnafahamu fika jinsi Serikali hii ya Awamu ya Tano ilivyo sikivu….umeniuliza malalamiko yaliyopo kwenye kipande hiki cha barabara kutokea Ilongelo-Mtinko-Mkalama kuanzia pale Igahule ilipoishia lami, na suala la wakulima wengi wa alizeti kushindwa kumudu gharama za kununua mbegu za kisasa kulingana na mahitaji ya soko, nataka nikuhakikishie vyote hivyo vipo mbioni kushughulikiwa,” alisema Katibu huyo wa Umoja wa Vijana.
Wakiwa katika shamrashamra za maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 43, Umoja huo wa Vijana ndani ya wilaya hiyo wamejikita katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo kupanda miti, kuwatembelea na kuwafariji watoto yatima na walio katika mazingira magumu.
Shughuli nyingine ni kufanya usafi wa mazingira, kujitolea damu kwa wagonjwa na wenye mahitaji, na kuunga mkono kwa kufukia kifusi kwenye shughuli ya ujenzi wa ofisi ya chama iliyopo Ilongelo
“Tunaomba wananchi wote muendelee kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi, ambacho ni dhahiri kinatoa mustakabali chanya wa ustawi kwa maendeleo ya mtu mmoja-mmoja na taifa kwa ujumla kuelekea uchumi wa kati,” alisema Zainabu Abdallah.