Walimu wa Kilimani Sekondari wakijumuika kwenye chakula cha mchana walichoandaliwa na kampuni ya URISINO Ltd kwenye hoteli ya WAG Hill baada ya shule hiyo kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.Picha zote na Baltazar Mashaka
.Mkurugenzi wa kampuni ya URISINO Ltd Mhandisi Mnandi Mrutu Mnandi, akizungumza walimu wa shule ya Kilimai Sekondari kabla ya hafla ya chakula alichowaandalia kuwapongeza kwa matokeo mazuri ya kidato cha nne.
Walimu wa Kilimani Sekondari wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa URISINO td Mhandisi Mnandi Mrutu Mnandi wa saba kutoka kushoto, baada ya hafla ya kuwapongeza iliyoandaliwa na mkurugenzi na kufanyika WAG Hill Hotel.Wa sita kutoka kushoto ni Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Ilemela Emmanuel Malima.
**********************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
MKURUGENZI wa kampuni ya URISINO Ltd, Mhandisi Mnandi Mnandi amesema uwekezaji wa serikali kwenye sekta ya elimu utumiwe na walimu wa shule za sekondari za umma kuvunja ufalme wa shule binafsi kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na kuiondolea serikali aibu.
Pia kampuni yake inatambua juhudi za serikali ya awamu ya tano mbali na kuboresha sekta ya elimu inaridhishwa na utendaji wa Rais John Magufuli hasa jitihada zake za kutoa elimu bure na kuhakikisha wanafunzi wa elimu ya juu wanapata mikopo.
Mhandisi Mnandi alitoa kauli hiyo kwenye hafla ya kuwapongeza walimu wa Sekondari ya Kilimani kwa matokeo mazuri ya kidato cha nne na cha pili mwaka jana, hafla iliyofanyika WAG Hill Hoteli jana.
Alisema atashirikiana na walimu wa Kilimani na wadau mbalimbali kuweka malengo ya kuondoa sifuri ili kuiunga mkono jitihada za serikali kuwapa elimu bora watoto wa wananchi masikini na kuhakikisha hakuna mwanafunzi atapata sifuri kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka huu.
Mhandisi Mnandi, alisema serikali ya awamu ya tano imeboresha na kujenga miundombinu ya shule mbalimbali ikiwemo Kilimani sekondari , kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne, huku wanafunzi wa vyuo vikuu wakinufaika na mikopo.
Alisema ili kuunga mkono juhudi hizo kampuni yake imejenga ofisi ya walimu, kulipa gharama ya Ankara ya umeme, gharama za kuunganisha huduma ya maji na kugharamia safari za mafunzo kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri ambapo sasa anakuja na mkakati wa kuondoa sifuri kwenye matokeo ya kidato cha nne.
“Niliguswa kuwa naweza kujitolea kuwa balozi wa Rais Magufuli ili kusaidia elimu kwa kutumia kipato kidogo ninachopata kwenye miradi inayotekelezwa na serikali kupitia kampuni ya URSINO Ltd ili kuifanya Kilimani sekondari kuwa shule bora nchini na 2020 bila sifuri Kilimani inawezekana,”alisema.
Mkurugenzi huyo wa URISINO alieleza kuwa serikali za awamu zilizopita zilifanya mengi lakini Rais Magufuli ameleta heshima kwenye elimu kwa kuwawezesha watoto wenye wazazi wasio na uwezo kusoma bure kwa usawa na hivyo walimu waisadie kuondoa sifuri na kuiondolea aibu hiyo kwenye matokeo ya mitihani.
“ Mwaka 2020 na kwa kuwa hatutaki kuona sifuri, tuliona tukae na walimu ili kuwapongeza na kuwaondoa kwenye dhana, tuwatoe katika mazingira yao, tuone tunafanya nini ili tupate matokeo chanya kwa kuondoa ziro,”alieleza Mhandisi Mnandi .
Alisema walimu wa Kilimani kwa mbinu za ufundishaji, wana uwezo wa kuvunja utawala wa shule binafsi na watoto wakifaulu vizuri ni faraja kwa walimu, wazazi na serikali, wakihitimu masomo yao ya kati na ya elimu ya juu watarudi kuitumikia serikali na kurejesha fedha zilizotumika kuwasomesha.
Mhandisi Mnandi alisema serikali inataka maendeleo na akawataka walimu kuacha ubinafsi bali washirikiane kuwachochea watoto kujifunza kwa bidii ili kuisaidia serikali na wananchi kuondoa aibu ya sifuri kwenye shule za kata za serikali ili kuonyesha zinaweza.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Ilemela, Emmanuel Malima, lengo la taasisi hiyo ya umma ni kupata mafanikio ya elimu kwa kuongeza ufaulu , hivyo ushiriki wa wadau ni muhimu kwani serikali pekee haiwezi.
“Ilemela tumempata ndugu,mdau na marafiki wa kweli kampuni ya URISINO.Ni kampuni inayojali walimu na kuwapa hamasa ili kuleta mafanikio ya elimu, kitendo cha kuwaleta hapa kitawapa nguvu kubwa ya kuongeza matokeo mazuri maana wanaona wanathaminiwa na hivyo watafanya kazi zaidi,”alisema Malima.
Naye Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo Atanass Manyika,alisema imekuwa na mafanikio makubwa ikishika nafasi ya 70 mwaka juzi kati ya shule 241 kimkoa na mwaka jana ilishika nafasi ya 47 kati ya shule 246 kimkoa ikiwa ni pili kwa shule za umma wilayani Ilemela.
Alisema Kilimani inaubeba mkoa wa Mwanza kwa shule za kata za umma ikiwa na wastani wa ufaulu wa asilimia 94.5 ambapo mwaka jana imeongeza ufaulu kwa wanafunzi wanne kupata daraja la kwanza, daraja la pili 24, la tatu 15, la nne 27 na wanafunzi 4 walipata sifuri.
Mmoja wa walimu wa shule hiyo Consolata Mosha kwa niaba ya wenzake aliahidi mwakani hawataki sifuri na malengo yao ni kupata ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi 30 na hivyo kila mmoja ajitathmini na kuimba “hatutaki ziro Kilimani.”