MABINGWA watetezi, Simba SC leo wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa Coastal Union mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Sasa Simba iliyo chini ya kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandonbroeck anayesaidiwa na mzalendo, Suleiman Matola inafikisha pointi 47 katika mchezo wa 18 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 11 zaidi ya Azam FC wanaofuatia katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 36 za mechi 17.
Kiungo Mbrazil, Gerson Fraga ‘Vieira’ ndiye ameibuka shujaa wa Simba SC leo baada ya kufunga mabao yote mawili, moja kila kipindi.
Fraga aliye katika msimu wake wa kwanza tangu asajiliwe Simba SC Agosti mwaka jana kutoka ATK ya India, alifunga bao hilo dakika ya nane kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo Mzambia, Clatous Chama.
Simba SC ikapata pigo dakika ya 37, baada ya beki wake mkongwe, Erasto Edward Nyoni kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na beki mpya, Kennedy Wilson Juma.
Gerson Fraga aliyewahi kuchezea pia klabu za Mumbai City ya India pia, na Renofa Yamaguchi ya Japan na Atletico Tubarao ya kwao, Brazil alifunga bao la pili dakika ya 78 akimalizia kazi nzuri ya kiungo wa kimatafa wa Tanzania, Hassan Dilunga.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Erasto Nyoni/ Kennedy Juma dk37, Tairone Santos, Gerson Fraga, Clatous Chama, Jonas Mkude, Meddie Kagere, John Bocco/Sharaf Shiboub dk82 na Ibrahim Ajibu/Hassan Dilunga dk63.
Coastal Union; Soud Abdallah, Hassan Kibailo, Omar Salum, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Ame, Salum Ally, Mtende Albano, Ayoub Lyanga, Shaaban Hamisi/ Hamad Majimengi dk69, Issa Abushehe na Ayoub Semtawa/Ayoub Semtawa dk89.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Kelvin Kongwe Sabato amefunga mabao yote dakika za 26, 88 na 90 Kagera Sugar ikiibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Singida United Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Namungo FC nayo ikaibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Mbao FC, mabao yake yakifungwa na Reliants Lusajo mawili dakika ya 34 na 79 na Hashim Manyanya dakika ya 45 Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Bao pekee la Vitalis Mayanga dakika ya 27 likapa Ndanda SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Alliance FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Biashara United imetoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Mwadui FC mabao yake yakifungwa na Mpapi Nasibu dakika ya 61 na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ dakika ya 80 kufuatia kutanguliwa kwa bao la Mussa Chamgenga dakika ya 38.
Ruvu Shooting ikaichapa Lipuli FC 3-1 mabao yake yakifungwa na Graham Naftari dakika ya sita, Rajab Zahir dakika ya 43 na Sadat Mohamed dakika ya 86 huku bao la wageni kutoka Iringa likifungwa na Daruweshi Saliboko dakika ya 53 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Mechi kati ya JKT Tanzania na Polisi Tanzania ilisitishwa dakika ya 53 timu hizo zikiwa hazijafungana kufuatia Uwanja wa Uhuru kujaa maji, wakati mchezo kati ya Tanzania Prisons na KMC haukufanyika kabisa sababu ya mvua kubwa.