Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Ujenzi Mrisho Mrisho, akifunga kikao kazi cha ndani cha Bodi ya Mfuko wa Barabara kilichofanyika kwa siku tatu mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Ujenzi Mrisho Mrisho (katikati), Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Utawala na Rasilimali Watu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Aureus Mapunda, wakati wa hafla ufungaji kikao kazi cha ndani cha wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara kilichofanyika mkoani Morogoro.
Viongozi na watumishi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, wakifuatilia kwa karibu hotuba ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Ujenzi Mrisho Mrisho (hayupo pichani), wakati akifunga kikao kazi cha ndani cha Bodi hiyo kilichofanyika mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Ujenzi Mrisho Mrisho, akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara mara baada ya kufunga kikao kazi cha ndani cha Bodi hiyo kilichofanyika kwa siku tatu mkoani Morogoro.
…..
WATUMISHI wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wametakiwa kuzingatia miongozo ya uandishi wa nyaraka mbalimbali za kiserikali ili kuboresha ubora na ufanisi wa mawasiliano ya kimaandishi ndani ya Serikali.
Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ujenzi Mrisho Mrisho, wakati akifunga kikao cha ndani chaWafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara kilichofanyika kwa siku tatu mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika utumishi wa umma .
Mrisho amesema miongozo hiyo inatoa viwango vya uandishi wa nyaraka kama vile uandishi wa barua za Serikali na una dhumuni la kuweka muundo wa pamoja katika mawasiliano ya kiserikali.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa watumishi wa Bodi hiyo kuboresha mahusiano na mawasiliano ndani ya Bodi ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga, ameeleza kuwa jumla ya watumishi 32 wameshiriki katika kikao hicho na kupata mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo na kuwaongezea ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kwamba watumishi hao pia wameapa na kutia saini viapo vya utunzaji siri za Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Mipango na Mapato kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara Godlove Stephen amesema watahakikisha wanayatekeleza vyema waliyojifunza hasa katika uandishi wa taarifa mbali mbali za Bodi kwa kuzingatia miongozo iliyopo pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya watumishi.
Naye, Afia Ndyamukama Mtumishi kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara ameiomba Bodi kutoa mafunzo kama hayo kwa watumishi mara kwa mara ili kuwajengea uwezo na kuwaongezea ufanisi zaidi katika utendaji kazi wao wa kila siku.