Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akizungumza na Wahitimu wa kada ya Famasi (Hawapo pichani) wakati wa warsha fupi ya kutoa vyeti vya kuhitimu na usajili iliyofanyika katika ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.
Mfamasia Mkuu Bw. Daud Mmasi akizungumza na wahitimu wa kada ya Famasi (Hawapo pichani) wakati wa warsha fupi ya kutoa vyeti vya kuhitimu na usajili iliyofanyika katika ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akimkabidhi mmoja wa wahitimu wa kada ya Famasi cheti cha taaluma pamoja na usajili katika warsha iliyofanyika jijini Dodoma.
Wahitimu wa kada ya Famasi wakila kiapo kilichoongozwa na msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe katika warsha ya kuwatunuku vyeti vya taaluma na usajili iliyofanyika leo jijini Dodoma.
*******************************
Na WAJMW-DOM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amewasihi wahitimu wa kada ya famasi kutoka vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi kuheshimu na kufuata misingi na miongozo ya taaluma hiyo ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Chaula amesema hayo mapema leo wakati alipohudhuria warsha fupi ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu na usajiri wahitimu zaidi ya 100 waliohitimu shahada ya Famasi katika vyuo mbalimbali nchini.
“Ninaomba mkawe wanyenyekevu mkiwa maeneo yenu ya kazi, kuzingatia kanuni na misingi ya taaluma ni jambo muhimu la kufuata kwa kila mmoja wetu, nidhamu mahala pa kazi huleta umakini katika kazi yako, jamii inawategemea ili muweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi”. Amesema Dkt. Chaula.
Dkt. Chaula ameendelea kusisitiza kuwa taaluma hiyo ni muhimu sana nchini kwani wagonjwa wanategemea kupata dawa sahihi ambazo zitatolewa na wafamasia hao ili ziwasaidie kupona maradhi yanayowasumbua.
Aidha, Dkt. Chaula amewataka Wahitimu hao kushirikiana kwa karibu na madaktari pamoja na wahudumu wengine wa afya wakiwemo manesi ili waweze kusaidia katika kutoa huduma bora za afya na kusaidia wananchi kupata nafuu na kupona kabisa maradhi yanayowasumbua.
Kwa upande wake Msajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth Shekalaghe amewataka wahitimu hao kwenda kuisaidia jamii na kuziba baadhi ya mapengo ya taaluma hiyo ambayo ina watumishi wachache na uhitaji ni kubwa nchini ambapo hivi sasa Tanzania ina wafamasia takribani 1200 waliosajiliwa na Baraza hilo nchi nzima.