
…………………………………………………………………………..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Umoja wa wazazi Tanzania( jumuiya ya CCM ) mkoa wa Arusha umeanzisha mpango maalumu wa kuchukua wanafunzi ambao hawakupangiwa kujiunga kwenye shule za serikali kutokana na alama zao kuwa chini ya 100.
Aidha umoja huo umelenga kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuhakikisha kila mtoto ambaye hakufanikiwa kuchaguliwa na serikali kujiunga kidato Cha Kwanza anaweza kuendelea kwa kupelekwa shule ya sekondari Leguruki iliyopo chini ya jumuiya ya CCM mkoani Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,Katibu wa wazazi mkoa wa Arusha,Ally Mussa Balloh alisema kuwa wamefikia hatua ya kuja na wazo hilo kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto ambao wamepata alama chini ya 100 katika matokeo ya darasa la Saba na kushindwa kuchukuliwa kujiunga na shule za serikali.
Alisema kuwa,wameshaanza kuzungumza na wazazi na wilaya ya Longido ambapo wamependezwa na utaratibu huo ambao unalenga kumkomboa kila mtoto kuweza kuendelea na elimu tena kwa gharama nafuu.
Naye Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Arusha ,Gerald Munisi alisema kuwa ,hivi Sasa wamejipanga kuzunguka wilaya zote za mkoa wa Arusha kwa ajili ya kuhamasisha wazazi kunufaika na programu hiyo ambayo inalenga kuwafikia watoto wote waliopata alama chini ya 100.
Munisi alisema kuwa, changamoto kubwa iliyopo ni kuwepo kwa mwamko mdogo wa elimu kwa baadhi ya wazazi ambapo kupitia mpango huo wameweza kuwahamasisha wazazi wilayani Longido na kuweza kupeleka watoto wao katika shule ya Leguruki.
Aliongeza kuwa,katika wilaya ya Longido jumla ya wanafunzi 362 wamepata alama chini ya 100 na kushindwa kuchukuliwa na serikali ambapo kupitia mpango huo wazazi wengi wameweza kuhamasika na kuanza mchakato wa kupeleka watoto wao katika shule hiyo.
“Hawa watoto wengi waliopata alama chini ya 100 sio kwamba hawana uwezo tunawachukua na kuwapeleka shuleni kwetu na kuweza kuandalia vizuri na mwisho wa siku hao wanafunzi ndio wanaokuja kuongoza katika nafasi za Kwanza darasani ,hivyo tunawaomba Sana wazazi wa wilaya zote za mkoa wa Arusha wachangamkie fursa hii kwani gharama zake ni kidogo Sana kwa mwaka na kila mzazi anaweza kumudu.”alisema Katibu Mwenezi .
Mwalimu mkuu wa shule hiyo,Emmanuel Loi alisema kuwa , kupitia mpango huo wamelenga kuchukua wanafunzi Mia mbili kwa mkoa wa Arusha ambapo mpango huo utakuwa endelevu lengo likiwa ni kuwasaidia watoto wote waliopata alama chini ya 100 na kushindwa kuchukuliwa na serikali kuweza kupata haki yao.
Loi alisema kuwa,kupitia mpango huo pia utaweza kwa kiasi kikubwa Sana kuwakomboa wasichana na wavulana wa jamii ya kifugaji ambao wengi wao wakishafeli hukimbilia kuozeshwa na wengine kwenda machungani ,hali ambayo mpango huo utaweza kuwakomboa na kuweza kuendelea na masomo yao kama kawaida kwa kujiunga na shule hiyo.