Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa(Mb), amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inajenga minara 38 kwa ruzuku ya shilingi, bilioni 7.1 Mkoani Kilimanjaro ikiwemo minara 6 inayojengwa katika wilaya ya Mwanga kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo ya vijijini wanapata huduma za mawasiliano ya uhakika.
Waziri Silaa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika kijiji cha Karamba Ndea, kata ya Toloha wakati wa ziara ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro, hususani katika lango la kuingia na kutoka watalii la Ndea kwenye hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Mhe. Silaa ameongeza kuwa, minara hiyo sita inayojengwa katika wilaya ya Mwanga, itasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa huduma ya mawasiliano ya simu katika lango hilo na kwa wananchi wa maeneo hayo kwa ujumla.
Akizungumzia wananchi kuunganishwa na huduma za mtandao wa intaneti, Mhe Silaa amesema, Serikali imekamilisha mradi wa kuiongezea uwezo (upgrade) minara 468 nchini iliyokuwa imejengwa kwa teknolojia ya kizazi ya pili (2G) ambayo hutoa huduma za kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi, kwenda teknolijia ya kizazi cha tatu na cha nne yaani (3G) na (4G), ambazo zinawezesha wananchi kutumia huduma ya intaneti kupitia simu zao.
Akizungumza kuhusu utatuzi wa changamoto za mawasiliano katika lango la Ndea, Mhe. Waziri alizielekeza UCSAF na TCRA kuhakikisha zinashirikiana na Watoa Huduma za mawasiliano kuhakikisha wanajenga mnara ili kutatua changamoto zilizopo. Pia alielekeza kuhakikisha kuwa maeneo mengine yaliyo ripotiwa na baadhi ya viongozi kuwa na changamoto za mawasiliano yanapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mwanga, Mhe. Mwanahamisi Munkunda amesema, uwepo wa mawasiliano ya uhakika katika wilaya hiyo utasaidia kukuza utalii na kuboresha uendeshaji wa shughuli za maendeleo na hatimaye kuchangia katika uchumi wa kidigitali.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Toloha, Mhe. Palesio Nalio ameshukuru Serikali kwa kuhakikisha minara hiyo inajengwa, huku akisisistiza kukamilika kwa miradi ya kuboresha usikivu wa redio pia kwa kuwa wananchi katika baadhi ya maeneo wamekuwa wakisikiliza redio za nchi jirani.
Serikali kupitia UCSAF inatekeleza mradi wa kimkakati wa ujenzi wa minara 758 inayojengwa katika kata 713 katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Kupitia mradi huo, Mkoa wa Kilimanjaro ulipata minara 38 ambapo mpaka kufikia tarehe 9 Aprili, 2025 jumla ya minara 20 ilikuwa tayari imewaka na inatoa huduma kwa wananchi. Kwa upande wa wilaya ya Mwanga, jumla ya minara sita inajengwa na minara 3 tayari imekamilika na inatoa huduma. Ujenzi wa minara 18 iliyosalia unaendelea na uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.