*Asema lengo ni kufungua fursa za kiuchumi na kijamii
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2025/2026 Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara za kimkakati zenye kufungua fursa za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa, nchi jirani na barabara za ulinzi kwa kiwango cha lami.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo miundombinu ya vivuko na madaraja ili kuunganisha maeneo ya nchi kavu ambayo yametenganishwa na maji katika maeneo ya bahari, maziwa na mito.
Ameyasema hayo juzi (Jumatano, Aprili 9, 2025) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Mtumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kwamba Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kutatua changamoto ya msongamano wa magari na kuboresha mfumo wa huduma za usafiri na usafirishaji katika majiji yenye msongamano ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Mbeya.
“Kwa upande wa Dar es Salaam, awamu ya tatu ya ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka kutoka Posta hadi Gongolamboto yenye kilomita 23.3 umefikia asilimia 80 na awamu ya nne ya ujenzi wa barabara ya Kivukoni hadi Tegeta ya urefu wa kilometa 30.1 umefikia asilimia 22.2.”
Waziri Mkuu alisema kwa upande wa Jiji la Dodoma, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje yenye urefu wa kilomita 112.3. Ujenzi wa sehemu ya kwanza kutoka Nala — Veyula — Mtumba — lhumwa Bandari Kavu (km 52.3) umefikia asilimia 84.72, na kwa sehemu ya pili kutoka lhumwa Bandari Kavu — Mtumba — Matumbulu — Nala (km 60) umefikia asilimia 81.5. “Kwa Jiji la Mbeya, ujenzi wa njia nne za barabara kutoka Nsalaga (Uyole) mpaka Ifisi (Kiwanja cha Ndege cha Songwe) yenye urefu wa kilomita 29 umefikia asilimia 22.”
Alisema mbali na ujenzi wa barabara pia Serikali katika mwaka 2025/2026 itaendelea na ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa; kuimarisha miundombinu ya bandari; kuimarisha Shirika la Ndege Tanzania; ukarabati wa meli zilizopo na ujenzi wa meli mpya; na kuendelea na ujenzi wa bandari kavu ya Kwala.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa reli, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa. “Hadi kufikia Februari, 2025 ujenzi wa kipande cha kutoka Mwanza – Isaka (km 341) umefikia asilimia 62.37; Makutupora – Tabora (km 368) umefikia asilimia 14.53; Tabora – Isaka (km 165) umefikia asilimia 6.33; na Tabora – Kigoma (km 506) umefikia asilimia 7.34.”
Mheshimiwa Majaliwa alisema maandalizi ya kuanza ujenzi wa kipande cha Uvinza – Malagarasi – Musongati (Km 282) yameanza ambapo Serikali za Tanzania na Burundi zilisaini mkataba wa ujenzi wa kipande hicho tarehe 29 Januari, 2025.