MABINGWA watetezi, Simba SC wameendelea kung’ara baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini Darves Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandonbroeck inafikisha pointi 44 katika mchezo wa 17 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi tisa zaidi ya Azam FC inayofuatia katika nafasi ya pili, ingawa imecheza mechi 16, wakati Namungo inabaki na pointi zake 28 za mechi 16.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Florentina Zabron wa Dodoma, aliyesaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga na Kassim Safisha wa Pwani, hadi mapumziko Simba SC walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-1.
Kiungo wa kimataifa wa Kenya, Francis Kahata Nyambura aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya 21 akiirukia kwa kichwa cha mkizi krosi maridadi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe kutoka kulia.
Mshambuliaji Mrundi, Bigirimana Blaise akaisawazishia Namungo FC dakika ya 35 akimalizia krosi ya beki Lucas Kikoti kutoka upande wa kushoto.
Kiungo Hassan Dilunga akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 38 kwa shuti la umbali wa mita 23 baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Namungo FC, kufuatia pasi ya mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere.
Kipindi cha pili Namungo walirejea na mipango mizuri na wakafanikiwa kuwabana vizuri wenyeji hadi walipopata bao la kusawazisha dakika ya 71 kupitia kwa Kikoti aliyepiga shuti la umbali wa mita 28 baada ya pasi ya Relliants Lusajo.
Hatimaye mshambuliaji kinara wa mabao wa Wekundu wa Msimbazi, Meddie Kagere akaifungia bao la ushindi Simba SC dakika ya 88 akimalizia pasi ya kiungo Msudan, Sharaf Eldin Shiboub.
Hata hivyo, wachezaji wa Namungo walimfuata refa kumlalamikia kwamba mfungaji wa bao hilo, Kagere alikuwa amezidi wakati anamchambua kipa raia wa Burkina Faso, Nourdine Balora, lakini mwanamama huyo aliwapuuza na akaweka mpira kat.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa/ Tairone Santos dk69, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Sharaf Shiboub, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/Cloutus Chama dk56 na Francis Kahata.
Namungo FC; Nourdine Balora, Miza Chrstom, Jukumu Kibanda, Carlos Protas, Stephen Duah, Daniel Joram/Paul Bukaba dk52, Hashim Manyanya, Lucas Kikoti, Bigirimana Blaise, Relliants Lusajo na George Makang’a/ Hamisi Khalifa dk59