******************************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Mkuu wa Mkoa Mtwara, Mhe. Gelasius Byakanwa amewaagiza Watendaji Kata na Vijiji kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani Wazazi na Walezi wote ambao hawajawapeleka Watoto shule mpaka sasa ambao wanaostahili kuanza darasa la kwanza na wale waliofaulu kidato cha kwanza.
Mhe. Byakanwa ameyasema hayo kwenye ziara ya siku aliyoifanya kwenye Tarafa ya Mihambwe ambapo alikuwa akikagua hali ya kuripoti Wanafunzi kidato cha kwanza pamoja na kukagua ujenzi wa miradi ya kimaendeleo kama vile Madarasa, Maabara pamoja na vyoo.
“Nawaagiza Watendaji Kata na Vijiji kuwakamata na kuwapeleka Mahakamani Wazazi na Walezi wote ambao wamekaidi utekelezaji wa kuwapeleka shule Watoto wao. Watakaokaidi kukamatwa Watendaji nijulisheni haraka, nitawashughulikia mwenyewe.” Alisisitiza Mhe. Byakanwa.
Kwenye upande wa ujenzi wa miradi ya maendeleo, Mhe. Byakanwa ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuvutiwa zaidi na utekelezaji wa kampeni aliyoianzisha ya ujenzi wa vyoo kwenye shule.
“Nilikuwa naona mitandaoni leo nimejionea mwenyewe, nakupongeza sana Afisa Tarafa Mihambwe Shilatu kwa kazi nzuri unayoifanya ya kusimamia miradi ya kimaendeleo. Nimevutiwa zaidi na namna ulivyosimamia kampeni ya shule ni choo, kote nilipopita nimeona kazi kubwa iliyofanyika. Hongera sana Shilatu.”* Alisema Mhe. Byakanwa alipokuwa akizungumza na Wazazi na Wananchi waliojitokeza Shule ya msingi Chikongo kilichopo Kijiji cha Chikongo kata ya Mkoreha wakati akihitimisha ziara yake ya siku moja alipotembelea Tarafa ya Mihambwe.