Katika mazungumzo yake Waziri Bashungwa amemtaka Bw. Nyaisa kuhakikisha analipa uzito wa kipekee suala la uboreshaji wa Mfumo wa Usajili kwa njia ya mtandao (ORS) pamoja na huduma kwa mteja ili kupunguza usumbufu kwa wadau.
“Ninakutaka ufanyiekazi mapungufu yote yaliyopo BRELA hasa upande wa mifumo na huduma kwa wateja ili kwenda na kasi ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli ya kuwa na Tanzania ya viwanda”.
Aidha Waziri Bashungwa amebainisha kwamba BRELA ni mlango wa wawekezaji na Wafanyabiashara hivyo huduma inapokuwa nzuri wateja wataongezeka pia mapato ya nchi yataongezeka.
Kwa Upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Nyaisa ametoa shukrani zake kwa uteuzi aliopata na kuahidi kufanya maboresho makubwa.
“Nakuahidi kujenga BRELA mpya itakayojibu mahitaji ya wadau wake wote kwa haraka. Nitumie fursa hii pia kuwajulisha wadau wote kuwa tunaandaa mkutano nao kwa nia ya kufahamiana, kupata maoni na ushauri wao katika kuijenga BRELA mpya”.
Bw. Nyaisa aliteuliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA tarehe 19 Januari, 2020 akichukua nafasi ya Bi. Loy Muhando aliekuwa akikaimu nafasi hiyo.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (kulia) akifanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa alipomtembelea katika Ofisi ndogo ya Wizara iliyopo waterfront Jijini Dar es Salaam ili kujadili dira mpya ya BRELA.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (kulia) akimkaribisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa (kushoto) mara baada kuwasili katika Ofisi ndogo ya Wizara iliyopo waterfront Jijini Dar es Salaam ili kujadili dira mpya ya BRELA.