Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Februari 6, 2025
ALIKUWA Mwalimu na Mke wa Rais, lakini safari yake haikukamilika kwa kuwa mke wa Rais.
Leo ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga,mkoani Lindi akiongoza kwa mfano na dhamira ya dhati.
Mama huyo, pia ni mwanasiasa ambaye ni mke wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, anaitwa Salma Kikwete na kwa takriban miaka ishirini akiwa mwalimu alifanya kazi kubwa katika sekta ya elimu.
Safari ya Mama Salma Kikwete ni ushuhuda wa jinsi ndoto, juhudi, na mapambano yanaweza kumpeleka mtu mbali zaidi ya alivyotarajia.
Kama mke wa Rais, ilikuwa ni chachu ya kumwezesha kufanya zaidi, na hiyo ndiyo ilimfikisha kuwa kiongozi mwenye nguvu katika ulingo wa siasa.
Akiwa Mbunge wa Jimbo la Mchinga, anajivunia kuwa kielelezo cha wanawake wanaoweza kutunga historia, na kuwa mfano bora kwa vijana, hasa watoto wa kike, wanaochipukia katika siasa.
WANAWAKE NA WASICHANA KUTHUBUTU KUGOMBEA
Akiwahimiza wanawake na wasichana kujikita kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi, Mama Salma anaeleza kuwa wanawake waliopo kwenye nafasi za maamuzi siyo wale waliobahatika tu, bali ni wale waliojizatiti kupitia ngazi za chini.
“Kwahiyo, bila kuanza hauwezi kufika, lazima tutafakari, tusitishwe, tusigombanishwe kwa kusema kwamba wewe ni mwanamke, utashindwa hapana!! simama imara,” anawasihi mama Salma.
“Mfano mimi mwenyewe, niliteuliwa kuwa Mbunge wa kuteuliwa mwaka 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tano, Hayati Dkt. John Magufuli ,hatimaye, nikaamua kuthubutu kugombea Jimbo kwa kuwa siku zote najiamini na dhamira ya kutaka kusaidia wananchi,” anaongeza.
Kwa mujibu wa Salma Kikwete, Jimbo la Mchinga ni kipande kidogo, lakini alianza kwa kiwango kikubwa katika Taifa zima, akiwa ameanzisha Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ili kumkomboa mtoto wa kike, hasa yule ambaye ni yatima na anayekulia kwenye mazingira magumu, lengo likiwa kumpatia haki ya elimu.
“Sio kwa kukosa baba au mama au bibi, ila ilikuwa kumpatia elimu nikimwaminisha kuwa namkomboa mtoto wa kike, napozungumza sasa wengi wamemaliza digrii, masters na wengine ni viongozi na wanafanya kazi maeneo mbalimbali,” anasisitiza Mama Salma.
“Mbunge wa Viti Maalum mkoani Pwani, Subira Mgalu, ni shahidi wakati ule alinisadia katika Taasisi ya WAMA, nilizunguka nchi nzima, walikuwa wakiniambia ‘Mama pumzika, Mama lala,’ lakini mimi niliwaambia sipumziki,” anasema mama Salma.
Mama Salma anaelezea kuwa, endapo asingeamua na kuweka uthubutu, asingefanikisha hayo kupitia Taasisi hiyo.
Anabainisha kuwa ,wapo wanawake wenye uwezo wa kuanzisha mambo makubwa ili kumkomboa mtoto wa kike au wanawake kwa ujumla, lakini wanakata tamaa.
Mama Salma anafafanua, wakati yeye anagombea Jimbo la Mchinga, alikatishwa tamaa na wengine wakisema kuwa hataweza kufika mbali.
“Wakati nagombea, yalisemwa mengi. Mara nilisemwa kuwa nipo ICU, nilisemwa sana, ‘Huyu anakwenda wapi? ameacha urais wa mume wake, anaacha nafasi aliyopewa” Hata mimi niliteuliwa na Rais Hayati Dkt. John Magufuli na isitoshe, alikuwa anateua vyombo, mimi ni chombo, lakini baada ya hapo, nikajitosa kugombea Jimbo,” anasema Mama Salma.
“Jimbo ambalo ni miongoni mwa mazuri, nawaambia hili, fuatilieni, nilishinda kura za maoni kwa asilimia kubwa na kwa bahati nzuri, kitu ambacho sitokisahau maishani ni kuhesabiwa kura hadharani, 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9… na niliwashinda wanaume niliogombea nao nipata kura 92 na nyingine zilizobakia waligawa”
“Ila kura zingehesabiwa ndani ningeambiwa ‘kura za itifaki.’ Mimi sikupata kura za kiitifaki, nilipambana na kufanya kazi hasa,” anasisitiza Mama Salma.
TAARIFA YA UCHAGUZI WA RAIS, WABUNGE, MADIWANI 2020 KUTOKA TUME HURU YA UCHAGUZI
Kati ya wagombea 15 wa kiti cha Rais walioteuliwa katika uchaguzi mkuu wa 2020, wanawake walikuwa wawili sawa na asilimia 13, na wanaume walikuwa 13 sawa na asilimia 87.
Kati ya wagombea 15 wa kiti cha Makamu wa Rais, wanawake walikuwa watano sawa na asilimia 33, na wanaume 10 sawa na asilimia 67.
Katika nafasi ya waliogombea Ubunge, wagombea walikuwa 1,257 katika majimbo 264, kati ya wagombea hao, wanaume walikuwa 964 sawa na asilimia 77, na wanawake walikuwa 293 sawa na asilimia 23.
Upande wa udiwani, wagombea walikuwa 9,231, kati yao 8,563 walikuwa wanaume sawa na asilimia 92.76, na 668 walikuwa wanawake sawa na asilimia 7.24.
MTANDAO WA JINSIA TANZANIA (TGNP) NA UN WOMEN
Akizungumzia takwimu ya wanawake kujitokeza kugombea nchini Tanzania, Gemma Akilimali, Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia (TGNP), anatoa rai kwa wasichana na wanawake kuwa na ujasiri na uthubutu wa kushiriki kugombea na kudai haki za wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Anaeleza kuwa wanawake wanaweza, kwani wanafanya kazi kubwa ya utekelezaji wa majukumu ngazi ya familia na wamekuwa wapangaji wazuri wa mipango ya raslimali na fedha katika familia.
Hata hivyo, Akilimali anasema kwamba, moja ya sababu zinazosababisha wanawake kushindwa kugombea uongozi na kufika ngazi za maamuzi ni mifumo kandamizi iliyopo kwenye jamii ambayo haimpi nafasi mwanamke kufanya maamuzi.
“Tanzania imeweka historia ya kuwa na Rais mwanamke kwa mara ya kwanza, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha dhamira ya kuongeza usawa wa kijinsia, na amekuwa mfano mkubwa na ushawishi kwa watoto wa kike,” anasema Akilimali.
Agnes Hanti, ni mratibu wa mradi wa kuwezesha wanawake katika Uongozi na Haki za Kiuchumi (WLER), akizungumza kwa niaba ya mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women), Bi. Hodan Addou, anaeleza kuwa mwaka 2022, shirika hilo, kwa msaada kutoka kwa Serikali ya Finland, lilizindua mradi wa miaka mitano wa “Kuimarisha Ushiriki wa Kusudi wa Wanawake na Wasichana, Uongozi, na Haki za Kiuchumi katika Ngazi ya Mitaa” (WLER).
Hanti anafafanua, lengo lilikuwa kuongeza ushiriki wa wanawake, ikiwa ni pamoja na wanawake vijana na walemavu, katika uongozi na majukumu ya kufanya maamuzi, na kukuza haki za kiuchumi za wanawake.
Anaeleza, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake ni hatua muhimu zaidi na yenye ufanisi katika kufikia usawa wa kijinsia.
“Tunapotafakari kuhusu ajenda ya Beijing+30, tuzingatie kuwa kukuza uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake si ndoto ya mbali, bali ni lengo la vitendo linalohitaji hatua thabiti katika ngazi zote,” anaeleza Hanti.
MAONI YA WANANCHI
Halima Abdul, msichana wa miaka 26, mkazi wa Yombo Bagamoyo, anaeleza kuwa mfumo dume unaoshuhudiwa kuanzia ngazi ya familia unamweka mtoto wa kike nyuma, na hivyo kumzuia kushiriki katika nafasi za uongozi na maamuzi.
Anaomba ,elimu ya usawa wa kijinsia itolewe kwa jamii, makanisa, miskiti, mashuleni kwa wanafunzi ili kila mmoja atambue kwamba hata mtoto wa kike ana nafasi ya kugombea na kutoa maamuzi.
Joseph Elinaza anaeleza, alitoa tahadhari kwa jamii kuondoa dhana kuwa mwanamke ameumbwa kuwa dhaifu hivyo ni rahisi kushawishika akiwa kiongozi.



