Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kufanya oparesheni, misako na doria zenye tija na kupata mafanikio ambapo kwa kipindi cha mwezi Februari jumla ya watuhumiwa 1108 walikamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali ikiwemo mauaji, kujeruhi, kupatikana na nyara za serikali, kupatikana na Pombe Moshi na kupatikana na dawa za kulevya.
WAKAMATWA WAKIWA NA NYARA ZA SERIKALI BILA KIBALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa Uhifadhi [TANAPA] wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha eneo la lyangoje Wilaya ya Mbarali wanashikilia watuhumiwa wanne, Isack Mahuvi [35] mkazi wa mlonga, Joseph Mhelela [45] mkazi wa Kijiji cha Chalisuka, Songa Kapunga [80] na Dogani Kapunga [70] wote wakazi wa Kijiji cha Igunda wakiwa na nyara za Serikali bila kibali.
Watuhumiwa walikamatwa wakiwa na vipande viwili vya meno ya tembo, kipande kimoja cha ngozi ya Nyati, miguu nane ya Swala, ngozi moja ya Swala, kichwa kimoja cha Swala na sikio moja la Swala. Watuhumiwa ni wawindaji haramu.
ASHIKILIWA KWA KUJIHUSISHA NA MATUKIO YA KUGHUSHI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Consolata Mwasege [47], mfanyabiashara, mkazi wa Ilomba Jijini Mbeya kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kughushi nyaraka mbalinbali.
Mtuhumiwa alikamatwa katika Mtaa wa Ilomba uliopo Jijini Mbeya na kukutwa na nyaraka mbalimbali zilizoghushiwa ambazo ni kadi 22 za NIDA za watu tofauti, kadi 04 za mpiga kura zenye majina ya watu tofauti lakini ukisikani QR Code inaonyesha jina la mtu mmoja kwenye kadi zote nne, vipeperushi vya matangazo ya freemason 200, kompyuta moja inayotumika kutengenezea nyaraka hizo za kughushi.
Mtuhumiwa amekuwa akighushi nyaraka hizo kwa kutumia kompyuta kwenye Stationary iitwayo CO Stationary kwa lengo la kujipatia kipato isivyo halali. Nyaraka hizo zimepelekwa Makao Makuu ya NIDA Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
WAKAMATWA WAKIWA NA NOTI BANDI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili Geofrey Braiton [29] na Michael Ruben [30] wote wakazi wa Mbeya mjini kwa tuhuma ya kupatikana na noti bandia za shilingi elfu kumi.
Watuhumiwa walikamatwa wakiwa katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Bondeni iliyopo Mtaa na Kata ya Itewe Wilaya ya Chunya wakiwa na noti bandia kumi na tano za shilingi elfu kumi [Tshs.10,000/=] kila moja ambazo kama zingekuwa halali ni sawa na shilingi 150,000/= zote zikiwa na namba CA 3903666.
Aidha, kwa kipindi cha mwezi Februari, 2025 jumla ya watuhumiwa 22 walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi kilogram 173.5, pia watuhumiwa 14 walikamatwa wakiwa na Pombe Moshi @ Gongo lita 68
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na jitihada za kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani kwa kuendelea kusimamia sheria za usalama barabarani, ukamataji wa makosa ya usalama barabarani na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya madereva wasio tii sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali.
Kwa kipindi cha mwezi Februari, 2025 jumla ya madereva 07 wamefungiwa leseni za udereva kutokana na kukiuka sheria za usalama barabarani kwa uzembe na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara na wengine kusababisha ajali za vifo na majeruhi. Aidha, kwa kipindi hicho jumla ya kesi 13 za ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani zilifikishwa mahakamani ambapo kesi zote 13 zilipata mafanikio kwa washitakiwa kutakiwa kulipa faini.
Kwa upande wa mafanikio ya kesi mahakamani, kwa kipindi cha mwezi Februari, 2025 jumla ya kesi zilizofikishwa mahakamani zilikuwa 748 kati ya hizo kesi 192 zilipata mafanikio mahakamani kwa watuhumiwa kukutwa na hatia na kuhukumiwa vifungo jela na wengine kulipa faini. Kesi 438 zipo mahakamani katika hatua mbalimbali.
AFUNGWA MAISHA JELA KWA KOSA LA KULAWITI.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya Mbeya imemhukumu Evaristo Angumbwike Mwakyoma [69] mkazi wa Mapelele Jijini Mbeya kwenda kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Mhe Teddy Mlimba na Mwendesha Mashitaka wa Serikali Rajabu Msemo Februari 25, 2025.
Mheshimiwa Hakimu Mlimba alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 154 cha sheria ya kanuni ya Adhabu, mshitakiwa Evaristo Angumbwike Mwakyoma [69] alitenda kosa hilo Aprili18, 2024 huko eneo la Mapelele Jijini Mbeya kwa mtoto wa Jirani yake mwenye umri wa miaka 05 baada ya kumlaghai.
Mhe Hakimu Mlimba ametoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa jamii na watu wengine wenye tabia kama ya mtuhumiwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kutii sheria bila shuruti na kujiepusha na vitendo vya uhalifu kwani havina nafasi katika jamii. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kufika mahakamani kutoa ushahidi katika mashauri mbalimbali yanayofikishwa mahakamani ili yaweze kupata mafanikio kwa watuhumiwa kutiwa hatiani na kutendewa kwa mujibuw a sheria.
Imetolewa na:
Kaimu Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.