Vijana wa Mtaa wa Uwanjani uliopo Kata ya Mwakakati Wilaya ya Momba Mkoani Songwe wametakiwa kukaa nyumbani baada ya kutoka shuleni na kuacha tabia ya kuzurura mitaani.
Kauli hiyo imetolewa Februari 27, 2025 na Polisi Kata ya Mwakakati Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Philipo Robert alipokutana na vijana hao na kuwashauri kuacha tabia ya kuzurura mitaani na kuwapa elimu ya umuhimu wa kuwasaidia wazazi na walezi kazi ndogo ndogo pindi warudipo shuleni ili waje kuwa wazazi na walezi bora katika maisha yao ya baadae.
“Acheni kuiga tabia ya baadhi ya vijana wenzenu ambao huwa wanacheza na kuzurura mitaani bila kuwa na kazi maalum ambazo zinawapelekea kujiingiza katika vitendo vya uhalifu na mwisho wao ufungwa jela” alisema Mkaguzi Robert
Aliongeza kuwa wapo baadhi ya vijana wanaoiga tabia ya baadhi ya vijana na watoto wa mitaani ambao wameshindikana na kujiunga kuwa marafiki zao kitendo ambacho kinapelekea kuanza kuiba vitu kwa wazazi na walezi na tabia hiyo hukua na kuanza kuiba kwenye mitaa mbalimbali na kuwataka kujiepusha na tabia hiyo kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.