…………………………………………………………………
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na Upanga imetwaa vikombe viwili vya ushindi na medali moja katika Mashindano ya Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Kampuni Binafsi za Tanzania (SHIMUTA) iliyofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa mwaka jana.
Ambapo timu ya Mloganzila kwa kushirikiana na upanga ilipata nafasi ya kushiriki michezo mbalimbali kama vile drafti, mpira wa miguu, riadha, bao, karata, visheli, mpira wa wavu, mpira wa pete na kukimbia na gunia na kufanikiwa kushika nafasi ya pili kwa upande wa mchezo wa drafti kwa wanaume ikiwakilishwa na Bruce Hassan na Basilisa Faranga nafasi ya tatu kwa wanawake na kisha kutwaa medali moja baada ya mchezaji Agnes Yasinti kukimbia mbio za mita 400.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vikombe hivyo Mwenyekiti wa Michezo MNH-Mloganzila, Bw. Goodluck Manji amesema kuwa ushindi huo waliupata kwa nyakati tofauti tofauti ambapo kwa upande wa wanaume walitwaa ushindi wakati walipofuzu kuingia fainali na nusu fainali kwa wanawake katika mchezo wa drafti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amesema amefurahishwa na ushindi huo na kuahidi kuwa uongozi wa hospitali uko pamoja na timu hiyo ili kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuangalia jinsi wanavyoweza kuwasaidia.
“Nimefurahishwa sana na ushindi huu mlioupata licha ya majukumu mliyonayo ya kuwahudumia watanzania na natambua ziko changamoto mbalimbali zinawakabili lakini uongozi wa hospitali uko tayari kuwasikiliza ili tuangalie jinsi tutakavyoweza kuwasaidia ili muendelee kufanya vizuri” amesema Prof. Museru.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi amewapongeza kwa ushindi waliopata na kuwasisitiza kuwa wasiishie hapo bali ushindi huo ukawe chachu ya kuongeza juhudi na kutwaa ushindi katika mashindano yajayo.
Baadhi ya timu zilizoshiriki ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Mamlaka ya Mapato (TRA), Mwanza UWASA, Mbeya UWASA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu Huria, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Hospitali ya Rufaa ya Bugando.