■Ahimiza Wazazi kusimamia elimu ya watoto wao ipasavyo
Na.Mwandishi Wetu -SUMBAWANGA
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe.Deus Sangu ameonesha kuumizwa na mwitikio mdogo wa elimu Mkoani Rukwa huku akiwaonya wazazi wenye tabia ya kuwaelekeza watoto wao kujikosesha au kuchora picha katika mitihani yao kwa lengo la kujihusisha na shughuli za kilimo na ufugaji.
Mhe.Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Kwela ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea na kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Miangalua iliyopo katika wilaya ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya elimu huku akitaja ujenzi Shule za Sekondari kila Kata pamoja na Shule ya Wasichana ya Rukwa, lengo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma.
Hata hivyo, Mhe.Sangu amesema kutokana na msukumo mdogo kutoka kwa wazazi, watoto walio wengi wamekuwa wakiishia darasa la saba na wale wanaoendelea na Sekondari wamekuwa hawafanyi vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho.
Kufuatia hali hiyo, Mhe.Sangu amesema Mkoa huo umekuwa kinara kwa idadi kubwa ya watoto wa kike kukatishwa masomo kutokana na kupata mimba, utapiamlo pamoja na tabia ya utapeli.
Amesisitiza kuwa elimu ndio injini ya maendeleo ya familia yoyote na kutoa angalizo kwa wazazi kuwa yoyote anayecheza na elimu ya mtoto wake atabaki kuwa nyuma huku fursa za kiuchumi za Mkoa huo zikiendelea kuporwa na wananchi wa Mikoa mingine.
” Mkoa wa Rukwa umejaaliwa rasilimali za kila aina ikiwemo madini pamoja kuwa ya pili kwa kuzalisha chakula lakini hali zetu ni duni kutokana na kukosekana kwa elimu” amesisitiza Mhe.Sangu
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Miangalua, Mhe.Didas Kayanda amesema jamii yoyote iliyostarabika ni lazima ikumbatie elimu, hivyo amewataka waumini hao kuwa mstari wa mbele kuwahimiza watoto wao juu ya umuhimu wa elimu.
Amesema wazazi ambao hawapeleki watoto shule wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe funzo kwa wazazi wengine huku akisema Serikali imejitahidi sana kujenga shule nyingi katika Jimbo la Kwela tofauti na hapo awali