Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Ujumbe wa Wabunge wa Bunge la Ulaya kutoka Kamati ya Ushirikiano na Maendeleo, kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam Februari 24.2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………..
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema jitihada za kujenga mahusiano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na nchi washirika zinazofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan zimekuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania.
“Tangu aingie madarakani Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara katika kujenga mahusiano na nchi mbalimbali jambo ambalo limeleta heshima kubwa na manufaa kwa nchi yetu hususan kwa kufungua fursa za kibiashara na uwekezaji kutoka nchi washirika”.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu Februari 24, 2025) alipokutana na ujumbe wa wabunge wa bunge la Ulaya (EU) kutoka Kamati ya Ushirikiano na Maendeleo kwenye Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amebainisha kuwa Umoja wa Ulaya umeendelea kuwa mdau mkubwa wa Tanzania katika kukuza biashara na uwekezaji kupitia nchi washirika. “Tanzania inathamini ushirikiano wa kiuchumi na kidemokrasia uliopo kati ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya.”
Amesema biashara baina ya Tanzania na nchi washirika wa Umoja wa Ulaya imeendelea kukua na nchi inanufaika kwa kupokea wawekezaji kutoka katika umoja huo.
“Uwekezaji wa nchi za Ulaya katika sekta ya kilimo, nishati, miundombinu, madini na utalii umekuwa kwa kiasi kikubwa. Pongezi zimwendee Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya ushirikiano huu.”
Kwa Upande wake, Mjumbe wa Bunge la Ulaya, Mheshimiwa Barry Andrews ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kazi kubwa inayofanya ya kuboresha maisha ya wananchi wake zikiwemo sekta za afya, elimu na miundombinu.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa ya maendeleo endelevu, ikiwemo utoaji wa huduma bora za afya, na elimu kwa wananchi.”
Amesema Umoja wa Ulaya utaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa Tanzania katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora .
“Katika miaka 20 iliyopita Tanzania imepiga hatua kubwa sana kwenye maboresho ya huduma za jamii na sasa kuna miundombinu bora ya usafirishaji inayochangia kukua kwa uchumi, Tunawapongeza sana.”
Ujumbe huo wa wabunge 14 wa Bunge la Ulaya uko chini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya Siku tatu na utakutana na Viongozi wa Serikali wadau wa maendeleo na wanufaika wa miradi inayoungwa mkono na Nchi washirika wa Umoja wa Ulaya.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Ujumbe wa Wabunge wa Bunge la Ulaya kutoka Kamati ya Ushirikiano na Maendeleo, kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam Februari 24.2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya picha ya simba Mwenyekiti wa Ujumbe wa Wabunge wa Bunge la Ulaya kutoka Kamati ya Ushirikiano na Maendeleo, Barry Andrews, kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, Februari 24.2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipeana mkono na Mwenyekiti wa Ujumbe wa Wabunge wa Bunge la Ulaya kutoka Kamati ya Ushirikiano na Maendeleo, Barry Andrews, kwenye ukimbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam Februari 24.2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Wabunge wa Bunge la Ulaya kutoka Kamati ya Ushirikiano na Maendeleo Barry Andrews, kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam Februari 24.2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)