Mkurugenzi wa Intelijensia ya jinai wa Jeshi la Polisi CP. Charles Mkumbo akipokelewa viongozi wa Kata ya Olasiti walifika kumpokea kwa ajili ya Mkutano na Wanachi wa Kata hiyo.
Mkurugenzi wa Intelijensia ya jinai wa Jeshi la Polisi CP. Charles O. Mkumbo akiongea na Wananchi wa Kata ya Murieti katika Mkutano maalumu kwa ajili ya kusikiliza maoni pamoja na changamoto ili kuweka mikakati ya pamoja kukomesha matukio kihalifu.
Diwani wa Kata ya Olasiti Bwana Alex Martin akitoa maoni yake katika kikao kilichofanyika katika kata hiyo kwa ajili kuweka mikakati ya pamoja ya kukomesha matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.
Mkazi wa Kata ya Olasiti Bi. Oliver Mbowe akitoa maoni yake katika kikao kilichofanyika katika kata hiyo kwa ajili kuweka mikakati ya pamoja ya kukomesha matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.
…………..
Na Gasto Kwirini wa Jeshi la Polisi Arusha
Mkurugenzi wa Intelijensia ya Jinai wa Jeshi la Polisi CP. Charles O. Mkumbo (DBCI) ametoa wito kwa Wananchi Jijini Arusha kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kukomesha matutiko ya ukatili dhidi ya wanawake yaliyojitokeza hivi karibuni Mkoani Arusha.
Wito huo aliutoa jana jioni wakati akizungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara ambao ulifanyika katika kata ya Olasiti na Muriet kwa lengo la kupanga mikakati ya pamoja katika kukomesha matukio ya kubakwa, kuporwa na kuuawa kwa Wanawake.
Alisema ni wakati wa jamii kutoa taarifa fiche za kuwafichua wahalifu kwakuwa tunaishi nao kwenye familia zetu. Jeshi la Polisi linategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa Wananchi katika kutekeleza majukumu yao kwani wahalifu wanaishi katika maeneo yao.
‘‘Tumekuja hapa ili tupate changamoto pamoja na maoni yenu ya nini kifanyike kwa sababu wahalifu wanaishi katika mitaa yenu kwani ni watoto wetu, wajomba zetu na hata wajukuu zetu, Ulinzi na usalama ni wajibu wa kila mwananchi na sio la Polisi pekee’’. Alisisitiza Kamishna Mkumbo.
Aliongeza kwa kusema Jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha Wananchi wanafanya shughuli zao katika hali ya usalama na kwamba upo uhitaji mkubwa wa kuwepo kwa ulinzi shirikishi kuanzia ngazi ya mitaa.
Naye diwani wa kata ya Olasiti Bwana Alex Martin alisema analishukuru Jeshi la Polisi Mkoani hapa kwa jitihada za haraka walizo zichukua baada ya matukio haya kutokea pamoja na ushrikiano ambao wamekuwa wakiutoa tangu kuanza kutokea matukio hayo.
Aliliomba Jeshi la Polisi kusaidia katika ujenzi wa kituo kidogo cha Polisi Olasiti, pamoja na kuipa hadhi ya Wilaya ya Kipolisi kata ya Muriet na Olasit ili kusaidia kupunguza au kumaliza matukio ambayo yamekua yakitokea kwani huduma ya Polisi itasogea karibu.
Naye Mkazi wa Olasiti Bi Oliver Mbowe alisema ni wakati sasa wa wazazi kukumbuka wajibu wao kwa familia na malezi bora kwa watoto wao ili kutokomeza uhalifu unaotokana na watoto wetu . Alisema kama wazazi watawalea watoto wao kwa maadili mema tatizo la uhalifu litaisha au kupungua kwa kiasi kikubwa.