Meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani Masawa Masatu,akizungumza wakati wa hafla ya siku ya shukrani kwa mlipa kodi kwa mwaka 2023/2024
NA VICTOR MASANGU, PWANI
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani imepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2023 /2024 baada ya kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 60.69 ikiwa ni sawa na kiwango cha utendaji wa asilimi 99.13 ambazo zimetokana na juhudi za kuwaelimisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari bila shuruti.
“Sisi kama Mamlaka ya Mapato Tanznaia (TRA) tumejitahidi sana katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara wetu juu ya umuhimu wa kulipa kodi ndio maana tumeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kukusanya kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 60 na kwamba watanzania wengi kwa sasa wamekuwa wazalendo kwani wanatambua umuhimu wa kulipa kodi ambayo inakwenda kuchangia kuleta maendeleo,”alisema Masatu.
Pia Masatu amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwa mzalendo na kutambua mchango wake mkubwa ambao anaufanya katika suala zima la kuhimiza ulipaji wa kodi kwa maslahi mapana kwa wananchi wa Tanzania ikiwemo pamoja na kuleta maendeleo katika nyanja mbali mbali.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanya biashara Mkoa wa Pwani Bundala Ndauka ameipongeza Mamlaka ya TRA kwa kuweza kuwapatia elimu mbali mbali juu ya umuhimu wa ulipaji wa kodi sambamaba na kuwawekea mazingira rafiki katika suala zima la utekelezaji wa majukumu yao.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika kilele cha maadhimisho ya siku ya shukrani kwa mlipa kodi kwa kipindi cha mwaka 2023 /2024 inasema kwamba kodi yetu maendeleo yetu
