Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) inasikitishwa na tukio la hivi karibuni lililotokea Unguja, ambapo imedaiwa kuwa Bi. Khadija Shaaban Ali (34) alimshambulia na kumjeruhi mke mwenzake kwa kumpiga visu, Bi Maimuna Said Suleiman (38), tukio lililomsababishia maumivu na majaraha makubwa.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo ZBC Radio kupitia kipindi cha Habari za Mawio kilichorushwa hewani tarehe 11 Februari 2025 ni kuwa wanawake hao walikuwa wamepakiwa katika gari moja na mume wao hadi nyumbani kwa mke mdogo huko Chukwani, mkoa wa mjini magharibi.
Kwa mujibu wa mawio mume aliingia ndani na kuwaacha wake zake hao wawili peke yao na ndipo mkasa huo ukaanza kutokea, ambapo taarifa zinadai kuwa Bi Maimuna alianza kupigwa kwa visu na kupiga makelele ya kuomba msaada lakini hata mumewe hakuweza kutoka kwa wakati.
TAMWA, ZNZ inasikitishwa na tukio hilo la Bi Khadija kumshambulia mke mwenziwe vibaya na kumsababishia madhara makubwa ya kimwili.
TAMWA ZNZ inasikitika zaidi na kitendo hicho cha mume wa wake hao kuondoka na kuwaacha peke yao bila ya hadhari zozote wakati yeye anawajua tabia zao vya kutosha.
Aidha inasisitiza kuwa hatua kali za kisheria zinahitaji kuchukuliwa dhidi ya wote waliohusika na kadhia hiyo ili iwe funzo kwa watu kujichukulia sheria mikononi mwao.
@TAMWA_Zanzibar www.tamwaznz.or.tz
TAMWA ZNZ inatoa ushauri kwa Serikali kuangalia uwezo wa wanaume wanaooa wake zaidi ya mmoja kama wana uwezo wa kutosha wa kuwahudumia na kuwalinda wake zao.
Pia inatoa wito kwa viongozi wa dini kujenga uelewa kwa jamii, hasa kwa wanaume juu ya wajibu wao wa kusimamia haki, usawa na amani katika familia zao.
Kwa mujibu wa rikodi za TAMWA ZNZ, tokea mwaka 2016, matukio 27 ya mauwaji ya wanawake na watoto yameripotiwa (wanawake 22 na watoto watano) na matukio zaidi ya 15 ya vipigo kwa wanawake tokea mwaka 2021, ambapo ni matukio machache yaliyopatiwa hatia za sheria.