***********************************
MUUNGANO wa Tanganyika na Zanzibar ambao tarehe 26 Aprili 2020 utafikisha miaka 56, umekuwa daraja lisilotetereka la kuwafikisha Watanzania katika azma yao ya kupata maendeleo, amani na ustawi.
Halikadhalika, Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015 – 2020, nayo inazielekeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa lengo la kuhakikisha Muungano unakuwa imara zaidi na kwamba amani na utulivu vinaendelea kuwepo nchini.
Katika kutekeleza maelekezo hayo ya Ilani, Januari 17 hadi 20 mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya ziara katika visiwa vya Unguja na Pemba ikiwa ni miongoni mwa harakati kuimarisha muungano na ushirikiano kati ya SMZ na SMT.
Akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu aliwakumbusha kuhusu kuenzi jitihada za waasisi wa Taifa hili yaani Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume za kutuunganisha kupitia muungano.
Alionya kuwa wananchi wasikubali kuhadaiwa na watu wachache wenye kupinga muungano kwani kwa kufanya hivyo watahatarisha amani ya nchi inayowafanya watembee kifua mbele na kuwa kimbilio la mataifa mengine yenye machafuko.
“Nchi yetu imepata mafanikio makubwa ya kuwa na amani na utulivu tangu tupate uhuru mwaka 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Imekuwa kimbilio la watu wa Mataifa ya jirani kila wapatapo matatizo ya uvunjifu wa amani katika nchi zao. Hivyo, hatunabudi kuienzi.”
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwahimiza Watanzania kushirikiana katika kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kamwe wasiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kuwagawa.
“Watanzania tusikubali mtu yeyote kutugawa kwa sababu sisi undugu wetu ni wa damu, hivyo ni vema tukaendelea kuudumisha muungano wetu tusiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kutugawa kwani nia za watu hao hazina tija.”
Waziri Mkuu aliongeza kuwa ni muhimu wananchi wakashirikiana na Serikali zote mbili katika kuyaendeleza mafanikio yaliyopatikana kutokana na uwepo wa muungano, kama uboreshwaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Pia waendelee kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha uchumi katika pande mbili za Muungano hususan katika kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manuafaa ya wananchi wa pande zote. “Muungano una tija kubwa kwetu sote tuulinde.”
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi wanazoendelea kuzichukua katika kuboresha maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili.
Aidha, mbali na kuwahamasisha wananchi hao washirikiane katika kudumisha muungano, pia Waziri Mkuu aliwataka wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda tunu yetu ya amani kwani suala la ulinzi ni jukumu la kila mmoja.
“Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi shirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi wa watalii na raia pamoja na mali zao ili kulinda hadhi ya mji huu ambao unatembelewa na watalii wengi.”
Mkuu wa mkoa na Viongozi wengine waimarishe umoja bila kujali itikadi za kivyama. Waziri Mkuu alisifu viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa walioshiriki kwenye ziara yake na kujionea wenyewe utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM.
Kadhalika, Waziri Mkuu akiwa kisiwani Pemba alikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za Polisi Mfikiwa, Chakechake na ujenzi wa nyumba za Polisi Finya. Alisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Akiwa katika mradi wa nyumba zilizopo Mfikiwa Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba sita za Askari Polisi zinazojengwa katika eneo hilo lililopo wilayani Chakechake. Kati ya nyumba hizo sita, tano tayari zimekamilika na zinatumika.
Nyumba moja ipo kwenye hatua za kukamilika. Pia, Waziri Mkuu alishuhudia matofali zaidi ya 32,000 katika eneo hilo la Mfikiwa ambayo yameshindwa kutumika kutokana na changamoto ya fedha. Ujenzi wa nyumba moja unakadiriwa kugharimu sh. milioni 35 iwapo zitajengwa kwa mfumo wa force account.
Kwa upande wa nyumba zinazojengwa katika eneo la Finya, nako kumejengwa nyumba tano za askari polisi ambazo licha ya kuwa zimeezekwa bado hazijakamilika ili kuanza kutumiwa na askari hao.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni kwa juhudi kubwa alizozifanya za kujitolea vifaa vya ujenzi vilivyosaidia kuanza kutekelezwa kwa miradi hiyo.
Aliongeza kuwa ni jukumu la wadau wengine nao kumuunga mkono ili kukamilisha ujenzi wa nyumba zilizobaki na kujenga nyumba nyingine kwa kutumia tofali zilizopo. Pia aliielekeza Wizara ya Mambo ya Ndani itenge fedha kwenye bajeti ijayo ya 2020/2021 kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo;.
“Makamanda wote wa Mikoa ya Polisi, wasipimwe na kuondolewa katika majukumu yao kwa kigezo cha kushindwa kujenga nyumba za askari iwapo hawajapewa fungu la kutekeleza miradi ya namna hiyo.
Katika hatua nyingine,viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani wakiwemo wa vyama vya CUF, NRA, UPDP, NSSR-MAGEUZI ambao walishiriki katika ziara ya Waziri Mkuu Zanzibar waliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuimarisha huduma za kijamii.
Viongozi hao walisema kuwa wapo tayari kushirikiana na Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais Dkt. Ali Mohammed Shein kwa sababu viongozi hao wanafanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahudumia wananchi. Pia waliahidi kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
“Maendeleo hayana chama naunga mkono jitihada zinazofanywa na SMT na SMZ na nimefurahia ziara ya Waziri Mkuu hapa kisiwani Unguja na ninamuunga mkono Rais Dkt. Magufuli tumepata maendeleo ambayo hatukuyatarajia,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa NRA Bw. Khamis Faki katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shehia ya Bambi.