MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameihoji serikali ni lini itawapatia leseni,mitambo na mitaji wachimbaji wadogo wa Jimbo la Singida Mashariki lililopo Mkoani Singida.
Mtaturu ameuliza swali hilo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Akijibu swali hilo,Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa amesema serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo ya uchimbaji kwa kuwatengea maeneo maalumu na kupitia mchimbaji mmoja mmoja kutuma maombi Tume ya Madini.
“Wachimbaji wadogo wa Jimbo la Singida Mashariki kama ilivyo kwa wachimbaji wengine wameendelea kupatiwa maeneo ya uchimbaji kupitia maombi ya mtu mmoja mmoja,pia kwa upande wa maeneo yanayotengwa, Mkoa wa Singida umetengewa eneo la Mhintiri, Londoni na Sambaru kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo,”.amesema.a
Katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitambo,amesema Serikali kupitia STAMICO imesaini Hati za Makubaliano (MoU) na Kampuni wazalishaji wa mitambo ya uchimbaji hapa nchini kwa lengo la kurahishisha upatikanaji wa zana na vifaa vya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo.
Kampuni hizo ni GF Truck, Appolo Heavy Equipments na META ambapo katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata vifaa STAMICO pia kupitia vituo vya mfano inakodisha vifaa vya uchimbaji kwa bei nafuu.
“Vifaa hivyo ni pamoja na compressor na water pumps,kuhusu upatikanaji wa mitaji ya kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo, STAMICO imeingia makubaliano na Taasisi za fedha za CRDB, NMB, AZANIA na KCB ili ziweze kuwakopesha fedha wachimbaji wadogo,”ameongeza Dkt.Kiruswa.
Aidha amesema Wizara kupitia STAMICO na Tume ya Madini imekuwa ikifanya semina na makongamano katika mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuwafahamisha wachimbaji wadogo juu ya fursa hizo.