![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/T1-1024x683.jpg)
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Stephen Wassira Akizungumza na Wanachama wa CCM wilaya ya Tarime, alipowasili katika ofisi za CCM wilayani hapo Katika Ziara yake ya kuimarisha chama Mkoani Mara. (Picha na CCM Makao Makuu )
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/T2-1024x683.jpg)
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Stephen Wassira Akizungumza na Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Wilaya ya Tarime, Leo Februari 08, 2025 (Picha na CCM Makao Makuu )
Na Mwandishi Wetu
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimedhamiria kuleta mapinduzi katika maisha ya wananchi kwa kuendelea kuwatoa katika hali duni na kuwajengea misingi ya maisha bora kwa kadiri inavyowezekana.
CCM imesema ukilinganisha na miaka 60 iliyopita Watanzania wa sasa wana hali bora Zaidi kutokana na kuimarika kwa maisha katika sekta mbali ikiwemo ya elimu na huduma za jamii.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyrkiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alipokuwa akizungumza na wana-CCM katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Wilaya Tarime, mjini Tarime, leo.
“Tunataka kufanya mapinduzi ya maisha ya watu na tunafanya, ndiyo maana watu wa Tarime sasa ni watu tofauti na waliokuwepo miaka 60 iliyopita. Unasimama unasema hatujafanya kitu, tumefanya, tumesomesha watu wengi sana hata wanaosema hatujafanya chochote tumewasomesha na uhuru wa kusema hatujafanya chochote tumewapa.
Alisema katika kipindi cha miaka minne pekee ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan serikali imeleta mabadiliko makubwa nchini ikiwemo wilayani Tarime ambako imejenga madarasa bila ya kuwachangisha wananchi kama ambavyo ilikuwa ikifanyika awali.
“Sisi ndiyo tunajenga maono ya TANU na ASP, sisi ndiyo tulijitoa muhanga kuondoa uonevu wa wakoloni katika nchi hii na tuna ajenda kubwa moja tu ya kuona maisha ya watu yanabadilika yanakuwa nafuu mwaka hadi mwaka, hiyo ndiyo kazi yetu na siyo kazi rahisi.
“Wako wengine wanasema CCM haijafanyika miaka 60, eti hatujafanya kitu, naomba muwasamehe kwa kuwa hawajui wanachosema, kwa sababu mimi kwa umri wangu nilikuwepo, niliijua Tarime kabla ya uhuru na nawaona wapo wazee hapa pia waliijua. Hii sura mnayoiona leo haikuwa sura ya Tarime ukiwarudisha watu wa Tarime wa mwaka 60 ukachukua na waliopo sasa hawawezi kuelewana, watu watarime wa sasa wote wanajua kusoma na kuandika lakini wa wakati ule walikuwa hawajui, akina mama wa Tarime sasa wanang’aa, akinamama wa Tarime wa wakati ule walikuwa wanatawaliwa na matatizo, hawakuwa na nguo za kuvaa.
“Kwa hiyo msisikilize maneno ya watu, sisi ni Chama Cha Mapinduzi, kuna vyama ni ugomvi na matusi tu…juzijuzi wamefanya mkutano wao Dar es Salaam pale wamegawana fito, mmoja kaenda na wake na mwingine kaenda na wake, kuna chama hapo? Sasa wanakuja kukwambieni Tarime muwapigie kura wamefanya kitu gani, maana mtu hupigi kura bila ya sababu,” alisema.
Wasira alikutana na wana CCM hao akiwa katika ziara yake ya kikazi kujenga Chama na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mkoani Mara.