Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ,akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu la Majengo na vituo vya daladala jijini Dodoma kupitia mradi wa uboreshaji miundombinu ya Miji (TACTIC) awamu ya pili unaotekelezwa chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA)
…….
OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ameagiza kufanyika tathmini ya Wakandarasi waliochelewesha miradi inayotekelezwa chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ambayo ilipaswa kukamilika Februari 2025 ili kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafungia wasipewe kazi ya popote.
Mhe. Mchengerwa ametoa agizo hilo katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu la Majengo na vituo vya daladala jijini Dodoma kupitia mradi wa uboreshaji miundombinu ya Miji (TACTIC) awamu ya pili unaotekelezwa chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Amemtaka Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seif na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo kufanya tathmini hiyo na kuagiza mkandarasi anayejenga barabara za jijini Dodoma asipewe kazi kutokana na kushindwa kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa.
“Haiwezekani Serikali kutoa Sh.bilioni 24 kwa ajili ya barabara, halafu watu wachache wanakwamisha jitihada za Mhe.Rais Samia. Iwe kampuni ya Kitanzania au ya kigeni, wasiwekewe tena mikataba hadi miradi yao yote iwe imekamilika,” amesisitiza.
Pia, ameelekeza TARURA kushughulikia haraka ujenzi wa kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 1.8 cha Iringa Road-Michese pamoja na barabara ya mita 750 eneo la Madukani na kwamba haiwezekani Makao Makuu ya Nchi yawe na barabara za changarawe.
Kuhusu changamoto za kuingia na kutoka katika Kituo cha Treni cha Reli ya Kisasa (SGR) jijini Dodoma, Waziri Mchengerwa amewaagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi wa Jiji na Mkuu wa Wilaya kukaa pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kuweka utaratibu mzuri wa usafiri kwa abiria.
Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema mradi huo utaboresha miundombinu muhimu ya Jiji hilo na kudai kuwa ujenzi wa vivuko utasaidia wanafunzi wa Mailimbili na Sechelela kuvuka makorongo wanapokwenda shule wakati wa mvua.
Awali, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seif, amesema miradi ya awamu ya pili jijini Dodoma, inayotekelezwa chini ya Mpango wa Kuboresha Miji 45 (TACTIC), ina thamani ya Sh. bilioni 14.2 na itachukua miezi 12 kukamilika.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vituo vya mabasi na daladala, uboreshaji wa Soko Kuu la Majengo, pamoja na ujenzi wa vivuko vya waenda kwa miguu.