Afisa Mahusiano wa Ruwasa Mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo kushoto,akiangalia sehemu ya kisima cha maji kitakachotumika kuhudumia wakazi zaidi ya 6.332 wa kijiji cha Angalia kata ya Mtina Wilayani Tunduru ambacho ni sehemu ya utekelezaji wa program ya uchimbaji wa visima 900 kila Jimbo visima 5,kulia Kaimu Mtendaji wa kijiji hicho Ramadhan Nyenje na katikati mkazi wa kijiji cha Angalia Yunusu Malemu.
Afisa Mahusiano wa Ruwasa Mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo kushoto na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Ruwasa Leticia Mwageni wa pili kushoto,wakimsikiliza Kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Angalia kata ya Mtina Wilayani Tunduru Ramadhan Nyenje kulia kuhusu maendeleo ya mradi wa maji ya kisima unaotekelezwa na Ruwasa unaotarajia kuhudumia wakazi zaidi ya 6,332 wa kijiji cha Angalia.
Na Mwandishi Maalum,Tunduru
WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA) Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,umeanza kutekeleza program ya uchimbaji visima 900/5 kwa kila Jimbo ambapo Wilaya hiyo yenye majimbo mawili ya Uchaguzi Tunduru Kusini na Kaskazini imepata mradi wa visima 10 vitakavyogharimu zaidi ya Sh.milioni 600.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Ruwasa Wilaya ya Tunduru Leticia Mwageni alisema,visima hivyo 10 vitachimbwa kwenye vijiji ambavyo hakuna miradi ya maji ya bomba kwa ajili ya kumaliza kero kwa Wananchi ya huduma ya maji safi na salama.
Mwageni alisema,miongoni mwa vijiji vilivyopata mradi wa kisima ni kijiji cha Angalia kata ya Mtina, mradi unaojengwa kwa kuwatumia mafundi wa ndani kwa gharama ya Sh.milioni 60.
Alisema,ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati,Ruwasa imenunua vifaa vyote vinavyohitajika na wameshaanza kujenga kituo cha kuchotea maji(kioski)na baada ya mwezi mmoja Wananchi wataanza kupata huduma ya maji safi na salama.
“Wilaya ya Tunduru ina majimbo mawili ya Tunduru Kusini na Kaskazini na mradi huu upo katika Jimbo la Tunduru ambalo limepata mradi wa visima 5 vinavyotekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 300 na Jimbo la Tunduru Kaskazini nalo tumepeleka visima 10”alisema Mwageni.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji wa kijiji cha Angalia Ramadhan Nyenje,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kupeleka mradi wa maji safi na salama katika kijiji hicho ambacho tangu Uhuru mwaka 1961 hakijawahi kupata maji ya bomba.
Nyenje alisema,Wananchi wa kijiji hicho wanafika zaidi ya 6,332 na wanategemea vyanzo vya asili kama mito na mabonde ili kupata huduma ya maji,hata hivyo havitoshelezi mahitaji kutokana na idadi kubwa ya watu waliopo.
Alisema,mradi wa kisima utawasaidia Wananchi kuondokana na adha ya kukaa muda mrefu kwenye mabomba machache ili kupata huduma ya maji na kwa kuwa mradi unajengwa karibu na Shule ya Msingi,Wanafunzi watapata maji safi na salama ya kunywa,maji kwa ajili ya kupikia na kufanya usafi wa mazingira
Hata hivyo,amewataka Wananchi kuhakikisha wanatunza mradi huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu kwani Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeonyesha mapenzi makubwa kwa wananchi wa kijiji hicho.
Mkazi wa kijiji cha Angalia Zena Ismail,ameiomba RUWASA kukamilisha ujenzi wa mradi huo haraka na kupeleka mabomba kwenye makazi yao ili waweze kuingiza maji majumbani badala ya kutumia vituo vya kuchotea maji.
“kwa sasa tunategemea kupata maji kutoka kwenye vyanzo vya asili ambayo maji yake siyo safi na salama lakini tunalazimika kuyatumia kwa kuwa hakuna huduma mbadala, hivyo mradi huu utatusaidia kuondokana na kero ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji”alisema.
Mkazi mwingine wa kijiji cha Angalia Rashid Zuber alisema,tangu mwaka 1994 walipopata visima vya kupampu kwa mkono ambapo baadhi vimeharibika hivyo,mradi huo utakuwa mombozi kwa kuharakisha maendeleo yao.