NA Francis Godwin, Iringa
Wafanyabiashara mbali mbali wilayani Mufindi mkoani Iringa wamesalimisha jumla ya kilo 344 za mifuko ya Plasitiki kwa ajili ya kuteketezwa ikiwa ni sehemu ya kutekeleza agizo la serikali la upigaji marufuku matumizi ya mifuko hiyo .
Akikabidhi mifuko hiyo kwa mkuu wa mkoa wa Iringa Alli Hapi jana wakati wa madhimisho ya siku ya mazingira duniani iliyofanyika katika viwanja vya mashujaa mjini Mafinga wilani Mufindi kwa mkoa wa Iringa, mkuu wa wilaya ya Mufindi Jamhuri Wiliam alisema kuwa mifuko hiyo imesalimishwa katika ofisi za Halmashauri na wafanyabiashara hao kabla kuanza kwa utekelezaji wa agizo la serikali na uzuiaji wa matumizi ya mifuko hiyo .
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wilaya ya Mufindi iliweza kutoa elimu kwa wananchi wake juu ya zuio la matumizi ya mifuko hiyo na hadi sasa wananchi wameanza matumizi ya mifuko mbadala inayotengenezwa na vikundi vya wajasiriamali kutoka ndani ya wilaya hiyo kwa kutumia karatasi kutoka kiwanda cha Mgololo kilichopo wilayani hapo .
” WAnanchi wetu wa Mufindi wameheshimu sana na kupokea maelekezo ya serikali ya kuanza matumizi ya mifuko mbadala lakini mkuu wa suala hili la mazingira ni pana sana na linagusa maisha ya wananchi wetu tunajua suala la kutunza vyanzo vya maji tumekuwa tukilipigia kelele na suala hili bado lipo na tumekuwa tukiwapigia kelele wananchi wetu kuhakikisha wanaacha hatua tano kutoka mito pindi wanapofanya shughuli za kilimo ”
Aidha alisema kuwa wilaya ya Mufindi wananchi wanatumia sana mkaa na kwa sasa kupitia viwanda mbali mbali vilivyopo wilayani Mufindi wameanza utengenezaji wa mkaa mbadala ambao tayari unauzwa kwenye maduka na maeneo mbali mbali ya wilaya ya Mufindi na nje ya wilaya hiyo japo bado kasi ya uzalishaji wa mkaa huo ni ndogo na haujaweza kuwatosheleza wananchi wengi.
Hivyo alisema wananchi wengi wameendelea kutumia mkaa wa miti ya porini na kuwa serikali haijapiga marufuku matumizi ya mkaa wa porini na kuwa wananchi wanaruhusiwa kuendelea kutumia mkaa wa porini na mkaa mbadala unaotengenezwa viwandani ila kinachotakiwa ni kufuata taratibu za ufanyaji wa biashara ya mkaa huo wa porini pasipo kuvunja sheria.
Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwataka wafanyabiashara na wananchi wa wilaya ya Mufindi kuendelea kutekeleza agizo la serikali la utumiaji wa mifuko mbadala na kuepuka matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo tayari imepigwa marufuku huku akiwataka wale ambao bado hawajasalimisha mifuko ya plastiki katika ofisi za Halmashauri ama ofisi za watendaji wa mitaa na kata kufanya hivyo kwani kukutwa na mifuko hiyo ni kosa kisheria na mtumiaji anaweza kufungwa jela siku saba ama faini .
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Iringa Alli Hapi mbali ya kupongeza hatua iliyochukuliwa na wafanyabiashara na watumiaji wa mifuko ya plastiki wilayani Mufindi kwa kukabidhi kilo 344 za mifuko hiyo kwa ajili ya kuteketezwa bado aliziagiza halmashauri zote za mkoa wa Iringa kuendelea kutoa elimu na kuwachukulia hatua wale wote ambao wanatumia mifuko ya plastiki mweupe kwa kufungashia bidhaa ambazo hazijawekewa nembo ya ubora na TBS .
Kuwa baada ya serikali kuzuia matumizi ya mikofo ya rambo na mingine ya plastiki yenye rangi baadhi ya wananchi wameanza kutumia mifuko ya plastiki mweupe kwa kugeuza kama kifungashio kuwa kufanya hivyo ni kosa na mifuko hiyo nayo haitakiwi ila vifungashio vinavyoruhusiwa ni vile ambavyo vimewekewa alama ya ubora na TBS pekee .
Alisema kutokana na na wajasiriamali wanawake katika wilaya ya Mufindi wameanzisha vikundi vya utengenezaji wa mifuko mbadala kwa matumizi ya kubebea bidhaa mbali mbali ni vizuri halmashauri za wilaya ya Mufindi kuwasaidia mikopo isiyo na riba ili kuongeza mitaji na kutafuta mashine za kutengenezea mifuko hiyo na ikiwezekana waweze kuisambaza wilaya nzima mkoa na nje ya mkoa wa Iringa .