Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera akizungumza wakati akifungua warsha ya siku tano kuhusu Uandaaji Mpangokazi wa uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (NSDI) jijini Dodoma jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Bw. Hamdouny Mansoor na kushoto ni Prof Elifuraha Mtalo.
Na Munir Shemweta, WANMM
Serikali imesema Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (National Spatial Data Infrastructure- NSDI) ni kiungo muhimu cha dira ya kimkakati ya uchumi wa kidigitali wa Tanzania 2024-2034 na kuchangia uchumi imara wa Taifa.
Uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (NSDI) ni jambo la kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera wakati wa uzinduzi wa warsha ya wataalamu ya kuandaa Mpango Kazi wa Uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (NSDI) jijini Dodoma.
‘’Kwa kifupi NSDI ni msingi wa kufanikisha malengo ya maendeleo ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 inayoandaliwa hivi sasa’’ amesema.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi, mfumo wa NSDI utaiwezesha nchi kujua kwa mapana ufanisi na mipango ya maendeleo, rasilimali zote za nchi na athari za mabadiliko ya tabia nchi, vikwazo vya uchumi na maendeleo ya nchi na kuboresha upatikanaji taarifa muhimu za kuimarisha mifumo ya usalama na uchumi wa nchi.
Aidha, Bi Kabyemera amesema, Sera ya Kitaifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) 2023 inasisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia kwa maendeleo ya jamii na kuichumi hivyo mfumo huo unalingana kikamilifu na sera hii kwa kutoa miundombinu ya data ya kijografia inayohitajika Mamlaka ya Serikali Mtandao ikiwa ni kiwezeshi muhimu katika kupanga na kuanzisha NSDI.
Akigusia Dira ya kidigitali ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2030, Bi Kabyemera amesema dira hiyo inalenga kuiweka Tanzania kuwa kinara wa mawasiliano ya kidigitali na Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijiografia ni kipengele muhimu cha dira hiyo kwa kuwa itawezeshwa kuunganishwa taarifa za kijiografia katika huduma mbalimbali za kidigitali.
‘’Mfumo huo utakaopoanzishwa utawezesha na kuhakikisha matumizi bora ya taarifa za kijografia kwa ajili ya kufanya maamuzi ya kupanga mipango mbalimbali katika sekta zote za maendeleo ya uchumi wan chi yetu’’ amesema Bi Kabyemera.
‘’Ni juhudi za pamoja za kuhakikisha kuwa taarifa za kijiografia zinapatkana kwa urahisui na kutumika kwa njia sahihi katika taasisi za serikali, mashirika ya umma, sekta binafsi na taasisi za elimu na utafiti’’ amesema.
Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za kijografia ni rasilimali muhimu kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi katika maeneo mbalimbali kama vile mipangpo miji, usimamizi wa maafa, kilimo na uhifadhi ya mazingira.
Uanzishwaji mfumo huo kutaweza kuboresha usahihi na ufanisi wa usimamizi wa ardhi, kusaidia usimamizi endelevu wa rasilimali za asili na ulinzi wa mazingira na kurahisisha mipango na uwekezaji wa msingi katika sekta za uchumi.
Warsha hiyo ya uandaaji Mpangokazi wa uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (National Spatial Data Infrastructure- NSDI) ni ya siku sita kuanzia Februari 3-7, 2025.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera akizungumza wakati akifungua warsha ya siku tano kuhusu Uandaaji Mpangokazi wa uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (NSDI) jijini Dodoma jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Bw. Hamdouny Mansoor na kushoto ni Prof Elifuraha Mtalo.
Sehemu ya washiriki wa warsha ya kuandaa Mpangokazi wa uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (NSDI) inayofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Hamdouny Mansoor akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tano kuandaa Mpangokazi wa uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (NSDI) inayofanyika jijini Dodoma.
Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya Upimaji na Ramani Dkt. Erick Mwaikambo akichangia mada wakati wa warsha ya ya kuandaa Mpangokazi wa uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (NSDI) inayofanyika jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera (Katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wanaoshiriki warsha ya kuandaa Mpangokazi wa uanzishwaji Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Kijografia (NSDI) jijini Dodoma jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)