MAOFISA kutoka Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (THBUB) wakiwapa elimu ya uelewa mapana juu ya dhana ya Haki za binaadamu na misingi ya Utawala Bora katika vyuo vya Mafunzo ya Amali vya Vitongoji na Daya, Pemba.
……
TUME ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (THBUB) imefanya ziara ya kuvitembelea vyuo viwili vya Mafunzo ya Amali vya Vitongoji, Wilaya ya Chake Mkoa wa Kusini Pemba na cha Daya Mtambwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, kwa lengo la kutoa elimu na kujenga uelewa mpana kwa jamii juu ya dhana nzima ya Haki za Binadamu na Misingi ya Utawala Bora.
Maafisa wa Tume hiyo, Ofisi ya Pemba wakiongozwa na Afisa Uchunguzi Ndg. Ramadhani Slaa wameifunza jamii juu ya umuhimu wa kutambua Haki za Binaadamu na Utawala Bora pamoja ushiriki na kuanzisha klabu za Haki za Binaadamu katika vyuo na kuwashauri wanafunzi wa vyuo hivyo kujiunga na klabu hizo.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, ofisi za chuo cha Vitongoji, Bw. Slaa alieleza nia ya ziara yao chuoni hapo mbali na kutoa elimu ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora lakini kushirikiana na vyuo hivyo kuanzisha Klabu za Haki za Binadamu na Utawala Bora ili kukuza ushirikiano na nguvu ya pamoja kwa kuongeza uelewa kwa jamii juu dhana ya Haki za Binaadamu na misingi ya Utawala Bora.
Aidha, Bw. Ramadhan Slaa awasihi wanafunzi vyuoni humo kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa jamii zao katika kueneza dhana halisi ya Haki za Binaadamu na misingi ya Utawala Bora ili kukuza jamii yenye uelewa mpana kwa maeneo hayo.
Katika hatua nyengine, THBUB ilimshauri, Mkuu wa chuo cha Daya cha Mtambwe, Mwl. Saada Ali Hamad, kuanzisha Klabu ya Haki za Binadamu na Utawala Bora chuoni hapo ili kuongeza hamasa na uelewa zaidi kwa jamii.
Naye, Mwalimu dhamana wa Chuo cha Mafunzo ya Amali cha Vitongoji na Mkuu wa Idara ya Masomo Mtambukwa chuoni hapo, Mwl. Khamis Abdalla Khamis alitoa shukrani kwa THBUB kwa kuwatembelea chuoni hapo sambamba na kuishauri Tume kuwa karibu na Klabu hizo ili kuzijengea uimara na ziwe endelevu pamoja na kuahidi kuzisimamia vyema katika kuendeleza shughuli za kutoa elimu kupitia klabu hizo.
Halikadhalika,kwa nyakati tofauti wanafunzi wa vyuo viwili hivyo, walipata nafasi ya kuuliza maswali kuhusu dhana na uelewa wa Haki za Binaadamu na Utawala Bora pia kutaka kujua umuhimu na faida za kujiunga na Klabu za Haki za Binadamu na Utawala Bora vyuoni humo.
Kwaupande mwengine, wanafunzi hao wameiomba THBUB kurudi tena kwenye vyuo vyao na kujenga utamaduni wa kuwatembelea mara kwa mara ili wajifunze zaidi. Hata hivyo, waliiahidi Tume kuongeza ushiriki wao mpana katika kusimamia na kuendeleza klabu hizo ndani ya vyuo vyao.
Kiasi cha wanafunzi wasiopungua 600 wakiwemo 400 kutoka Chuo Cha mafunzo ya Amali cha Vitongoji na 200 kutoka chuo cha Daya, Mtambile kwa nyakati tofauti walihudhuria hafla hiyo iliyowajenga kitaaluma na kuelezwa juu ya umuhimu wa kushiriki klabu kama hizo na umuhimu wake wa kuanzishwa kwenye vyuo vyao.
WANAFUNZI wa Chuo Cha Mafunzo ya Amali Vitongoji Wilaya ya Chake, Mkoa wa Kusini Pemba wakiwasikiliza Maofisa kutoka Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (THBUB) juu ya uelewa mpana wa dhana ya Haki za binaadamu na misingi ya Utawala Bora
WANAFUNZI wa Chuo Cha Mafunzo ya Amali wa chuo cha Daya, mtambile, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba wakiwasikiliza Maofisa kutoka Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (THBUB) juu ya uelewa mpana wa dhana ya Haki za binaadamu na misingi ya Utawala Bora.
MAOFISA kutoka Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (THBUB) wakiwapa elimu ya uelewa mapana juu ya dhana ya Haki za binaadamu na misingi ya Utawala Bora katika vyuo vya Mafunzo ya Amali vya Vitongoji na Daya, Pemba.